Kahata rasmi Simba, Okwi sasa basi tena

05Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kahata rasmi Simba, Okwi sasa basi tena
  • ***Sasa bado nafasi moja tu ya nyota wa kimataifa, Zana Coulibaly akaribia kuiziba huku ikielezwa...

WAKATI mashabiki na wanachama wa Simba wakiwa bado na kiu ya kumuona mshambuliaji wao, Mganda Emmanuel Okwi akiitumikia klabu hiyo, uwezekano wa kusaini mkataba mpya unaelekea kuyeyuka baada ya kumnasa kiungo wa kimataifa wa Kenya Francis Kahata.

Kahata aliyetua jana Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, tayari ametangazwa kujiunga na mabingwa watetezi hao wa Ligi Kuu Bara na hata kabla ya kutangazwa alishaandika kwenye wikipedia kwamba yeye ni mchezaji wa Simba kuanzia mwaka 2019.

"Ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kucheza eneo la kiungo, kwa sasa akiwa sehemu ya wachezaji wanaounda kikosi cha timu ya Taifa ya Kenya kilichoshiriki Afcon, Francis Kahata (27), msimu ujao atavaa jezi ya mabingwa wa nchi baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili.

"@kachikahata amejiunga Msimbazi akitokea Gor Mahia ya Kenya ambapo akiwa kwenye klabu hiyo alishinda Kombe la Ligi Kuu mara tatu, Kiungo Bora wa mwaka wa Ligi Kuu ya Kenya mara mbili na Mchezaji Bora wa msimu 2018/2019 wa Gor Mahia. #Nguvu Moja," ilieleza taarifa ya Simba kupitia ukurasa wao wa Instagram jana.

Kutua kwa Kahata aliyezaliwa Mei 4, 1992, ina maana Simba sasa imefikisha jumla ya wachezaji tisa wa kigeni, sita wapya na watatu walioongezewa mikataba yao hadi sasa kwa maana hiyo kunaifanya kubakiwa na nafasi moja tu ya nyota wa kigeni kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu Bara ambazo zinataka kila klabu kutozidisha nyota 10 wa kigeni.

Kuelekea msimu mpya wa 2019/20, tayari Simba imeshanasa saini za wachezaji wapya sita wa kigeni, ambao ni mabeki Wabrazil Gerson Fraga Vieira kutoka ATK ya Ligi Kuu ya India na Tairone Santos da Silva kutoka Klabu ya Atletico Cearense FC, mshambuliaji Wilker Henrique da Silva kutoka Bragantino, zote za Daraja la Nne nchini Brazil na viungo Msudan Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman aliyetokea Al Hilal ya Sudan pamoja na winga Deo Kanda kutoka TP Mazembe ya kwao, DR Congo na sasa Kahata kutoka Gor Mahia.

Nyota hao wapya sita wanaungana na wachezaji watatu wa msimu uliopita ambao wameongezewa mikataba mipya, kiungo Mzambia Clatous Chama, straika Mnyarwanda Meddie Kagere na beki Muivory Coast Pascal Wawa, hivyo kufikisha jumla ya wachezaji wa kigeni tisa.

Lakini kwa sasa beki wa pembeni, Zana Coulibaly, yupo nchini akifanya mazungumzo ya kuongeza mkataba na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, hivyo kama dili hilo likikamilika ina maana Okwi ndio basi tena ndani ya kikosi hicho cha mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Kahata alianza kuichezea Harambee Stars kwa mara ya kwanza mwaka 2011 na hadi sasa ameshaitumikia jumla ya mechi za kimataifa 31.

Alianzia soka lake Thika United ambapo aliichezea akiwa kinda kabla ya kuanza kucheza timu ya wakubwa mwaka 2008–2015 na kisha mwaka 2010 kutolewa kwa mkopo University of Pretoria, huku mwaka 2014 akiitumikia KF Tirana kwa mkopo kabla ya mwaka unaofuata kusaini jumla, na kuanzia mwaka 2015–2019    alikuwa akikipiga Gor Mahia.  

 

Habari Kubwa