Kakolanya rasmi asajiliwa Simba

15Jun 2019
Somoe Ng'itu
DAR
Nipashe
Kakolanya rasmi asajiliwa Simba
  • ***Ni baada ya kuitingisha Yanga ambayo leo inaendesha harambee ya "Kubwa Kuliko"...

WAKATI mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wakiendelea kuimarisha kikosi chao kwa kunasa saini ya kipa, Beno Kakolanya, watani zao Yanga leo wanatarajia kufanya harambee ya kihistoria ili kukusanya fedha kwa lengo la kusajili wachezaji watakaowatumia kwenye msimu ujao.

Mabingwa hao wa Bara, jana mchana walitangaza kumsajili Kakolanya, ambaye alikuwa mchezaji huru kwa kumpa mkataba wa miaka miwili.

Kakolanya alitangazwa kuwa huru baada ya Yanga kushindwa kumlipa malimbikizo ya mshahara wake na hivyo kuamua kukaa pembeni.

Kipa huyo atatakiwa kupambana kuwania namba dhidi ya mlinda mlango chaguo la kwanza la Wekundu wa Msimbazi, Aishi Manula na Deogratius Munishi "Dida" ambaye mpaka sasa hatima yake kikosini hapo haijajulikana.

"Ni Beno Kakolanya. Hakuna ubishi kuwa huyu ni moja ya makipa wenye uwezo mkubwa nchini na tunaamini akishirikiana na wenzake katika kikosi chetu, watatuwezesha kuongeza ukubwa wa timu na kutupatia mataji zaidi msimu ujao, tumemalizana naye," alisema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori.

Kiongozi huyo alisema kuwa Simba imejipanga kuimarisha safu zote katika kikosi chake kwa sababu inataka kupata mafanikio zaidi katika mashindano ya kimataifa ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Taarifa zaidi kutoka Simba zinasema kuwa tayari wamefanikiwa kumrejesha beki, Miraji Athumani ambaye msimu uliopita alikuwa katika kikosi cha Lipuli FC ya mkoani Iringa.

 

MAJALIWA, KIKWETE NDANI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuongoza harambee ya klabu ya Yanga iliyopewa jina la "Kubwa Kuliko" itakayofanyika leo kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya harambee hiyo, David Ruhago, alisema jana kuwa maandalizi yamekamilika na alimtaja Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete naye anatarajiwa kuhudhuria akiwa ni mgeni maalumu.

"Hii ni fursa adimu kwa kila Mwanajangwani kupata nafasi ya kujumuika na Wanayanga wengine katika harambee hii yenye lengo la kuirudisha Yanga mahali pake," alisema Ruhago.

Alisema kuwa wanaamini baada ya harambee hiyo, Yanga itarejea katika hadhi na ushindani kwa kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano yote watakayoshiriki.

Habari Kubwa