Kampira aitabiria Yanga makubwa msimu ujao

21May 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR
Nipashe
Kampira aitabiria Yanga makubwa msimu ujao

WACHEZAJI wa zamani wa Yanga, wamesema wanaamini kuwa kikosi chao kitakachoshiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao kitakuwa na timu imara na kitafanya vema kwenye mashindano mbalimbali watakayoshiriki.

Mwenyekiti mpya wa klabu hiyo, Dk. Mshindo Msolla

Kauli hiyo imetolewa siku chache baada ya Mwenyekiti mpya wa klabu hiyo, Dk. Mshindo Msolla, kutangaza kuwashirikisha nyota hao katika mchakato wa kusajili wachezaji.

Msolla alisema ili kuwa na kikosi imara, uongozi wa klabu hiyo utampa jukumu la usajili Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera pamoja na nyota hao wa zamani ili kukamilisha mchakato huo kwa kuwakabidhi fedha za usajili.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Umoja wa Wachezaji wa zamani wa Yanga, Ramadhani Kampira, alisema uamuzi huo umewafurahisha na anaamini utaifanya timu yao kuwa bora na itakayoshinda mataji mbalimbali katika msimu ujao.

Kampira alisema wao wanawafahamu wachezaji wenye uwezo wa hapa nchini na vile vile kiufundi watamsaidia Zahera kusajili wachezaji watakaokuwa na msaada kwa Yanga na si wale watakaokuja kujaribu "bahati".

"Tunafurahi kupata nafasi hii, miaka ya nyuma wachezaji walikuwa wanasajiliwa kwa kubahatisha, tunaamini kwa ushirikiano huu, mambo yatakuwa mazuri na Yanga itakuwa tishio," alisema Kampira.

Aliongeza kuwa kwa uamuzi huo, wala Yanga haitatumia kiasi kikubwa cha fedha ili kukamilisha mchakato huo na badala yake kamati hiyo mpya itasajili kwa kuzingatia viwango.

Mbali na Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ambayo inaombea Simba ipoteze mechi zake zilizosalia na yenyewe kushinda michezo yake miwili iliyobakia, itashiriki Kombe la FA, Kombe la Mapinduzi na Kombe la SportPesa.

Habari Kubwa