Kamusoko, Ajibu waamsha "mzuka" 

09Feb 2018
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kamusoko, Ajibu waamsha "mzuka" 

WAKATI kesho ikitarajiwa kuivaa St Louis katika mchezo wa kwanza hatua ya awali ya mashindano Ligi ya Mabingwa Afrika, nyota, Thaban Kamusoko, Ibrahim Ajib na Youthe Rostand, wamekoleza mzuka wa Yanga kuwavaa Washelisheli hao.

Ibrahim Ajib

Nyota hao ambao walikuwa nje wakiuguza majeraha, jana asubuhi walifanya mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzao na habari njema kwa mashabiki wa timu hiyo ni kuwa wanaweza kucheza katika mchezo huo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

Mbali na wachezaji hao, pia mabeki, Juma Abdul na Andrew Vincent "Dante" hali zao ni "fiti" baada ya kupona majeraha yao.

Meneja wa timu hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa, Hafidh Saleh, ameliambia Nipashe jana kuwa, nyota hao wote wamefanya mazoezi kamili na wachezaji wenzao.

“Tunashukuru kwa kweli kuelekea kwenye mchezo wa Jumamosi (kesho) baadhi ya wachezaji wetu wamepona majeraha yao na wamefanya mazoezi na wenzao,” alisema Saleh.

Aidha, Kocha Msaidizi, Shadrack Nsajigwa, alisema suala la kucheza au kutokucheza kwa wachezaji hao litaamuliwa na Kocha Mkuu, Mzambia, George Lwandamina.

“Kupona kwao kutatuongezea nguvu, tulikuwa katika wakati mgumu wa kukabiliana na hali ya majeruhi,” alisema Nsajigwa.

Hata hivyo kuna uwezekano mkubwa Ajibu na Rostand wakaanza kwenye mchezo wa kesho, lakini Kamusoko akitarajiwa kusubiri hadi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Majimaji utakaofanyika Februari 14 mwaka huu.

 

 

Habari Kubwa