Kamusoko kuwavaa Kagera leo

09Mar 2018
Faustine Feliciane
Nipashe
Kamusoko kuwavaa Kagera leo

YANGA leo inashuka uwanjani kuumana na Kagera Sugar kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara huku kiungo wake, Thaban Kamusoko akitarajiwa kurejea uwanjani baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha.

Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh.

Mchezo huo awali ulipangwa kufanyika kwenye uwanja wa Taifa, lakini kuna uwezekano ukachezwa kwenye uwanja Uhuru.

Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, aliiambia Nipashe jana kuwa Kamusoko ameshapona majeraha yake lakini hakupangwa kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa Ulaya Jumanne iliyopita kwa kuwa hakuwa fiti kwa asilimia miamoja.

"Kesho (leo) Kamusoko anaweza akacheza lakini si kwa dakika zote 90, ametoka kuwa majeruhi hivyo atapewa muda mdogo ili kuendelea kuimarika," alisema Saleh.

Endapo Yanga itafanikiwa kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa leo, itakuwa imepunguza pengo la pointi baina yao na vinara Simba na kufikia pointi tatu na kuendelea kuchochea ushindani kwenye kuwania ubingwa msimu huu.

Yanga leo itawakosa, kiungo Raphael Daud na Geofrey Mwashiuya ambao wana kadi tatu za njano.