Kaseba aendelea kujiweka imara

21May 2020
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Kaseba aendelea kujiweka imara

BONDIA aliyejipatia umaarufu nchini kupitia mchezo wa Kick Boxing, Japhet Kaseba, amesema anaendelea na mazoezi kwa lengo la kuboresha kiwango chake.

BONDIA Japhet Kaseba:PICHA NA MTANDAO

Akizungumza na gazeti hili jana, Kaseba ambaye aligeuka na kuwa bondia wa ngumi za kulipwa alisema anatambua madhara ya kukaa muda mrefu bila ya kufanya mazoezi.

Kasema alisema katika kipindi hiki ambacho serikali imesimamisha michezo, yeye anaendelea kujiimarisha kwa sababu anataka kulinda kiwango wake kwa kuupa mwili wake mazoezi kama ilivyokuwa zamani.

"Ninakitendea haki kipaji changu kwa kuendelea kufanya mazoezi kila siku, kipindi hiki nakitumia vizuri kujinoa kwa nguvu huku wanamichezo wote tukisubiri tamko la serikali kama michezo itaendelea kuchezwa au la," alisema Kaseba.

Amewataka mabondia wote wa hapa nchini kutobweteka na kuwakumbusha wakifanya hivyo watashusha viwango vyao na kujiweka kwenye hatari ya kuua vipaji walivyonavyo.

" Nimefarijika na kupata matumaini baada ya kusikia serikali inafikiria kurudisha michezo, uamuzi huu umenifurahisha kwa kiasi kikubwa, naamini kila mmoja hakuacha mazoezi," alisema Kaseba.

Alishauri endapo tarehe ya kuanza kwa michezo itatangazwa, wachezaji wote wapimwe kwanza kabla ya kuendelea tena na mashindano.

Habari Kubwa