Kaseja kuula Kagera Sugar

14May 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe Jumapili
Kaseja kuula Kagera Sugar

UAMUZI wa kipa Juma Kaseja kubaki au kuendelea kuitumikia Kagera Sugar katika msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara uko mikononi mwake, imeelezwa jana.

Juma Kaseja.

Kaseja kipa wa zamani wa Moro United, Simba na Yanga, alijiunga Kagera Sugar kwa mkataba mfupi akitokea Mbeya City ya jijini Mbeya.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Kagera Sugar, Mohammed Hussein alisema uongozi na benchi la ufundi la timu hiyo umeridhishwa na kiwango alichokionyesha na wangependa kuona anaitumikia klabu hiyo katika msimu mwingine.

Mohammed alisema wanaamini wakiongeza wachezaji wachache, msimu ujao timu yao itakuwa moja ya klabu zitakazokuwa zinawania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya Kombe la FA.

"Kiukweli msimu ujao tunataka tuwe na kikosi imara zaidi, kwa upande wa Kaseja bado tunamhitaji katika timu yetu, na wachezaji wengine tutawapa mikataba mipya, tunaamini tusipomeguka, hatutakamatika msimu ujao," alisema kiongozi huyo.

Kaseja alirithi nafasi iliyoachwa na kipa Hussein Shariff 'Casillas' ambaye alisimamishwa kwa muda usiojulikana baada ya kutuhumiwa kuihujumu timu kutokana na kukubali kichapo cha mabao 6-2 wakati walipoikaribisha Yanga kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza.