Katwila aitabiria mazuri Ihefu FC

21Nov 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Katwila aitabiria mazuri Ihefu FC

WAKATI leo watakuwa ugenini kuwavaa Polisi Tanzania, Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Zuberi Katwila, amesema hatakuwa tayari kuiona timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara inashuka daraja na kuahidi kutumia ujuzi wake wote ili kusalia kwenye ligi hiyo.

Kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, alisema kipindi cha mapumziko ya kupisha kalenda ya kimataifa, alikitumia kurekebisha makosa aliyoyabaini kwenye kikosi chake baada ya kutua katika timu hiyo ya jijini Mbeya.

"Katika mapumziko haya nimekaa na vijana na kurekebisha vitu kadhaa na natumaini kwenye mechi zinazokuja tutapata matokeo mazuri," alisema Katwila, mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar ya Manungu mkoani Morogoro.

Alisema kila mechi wanayocheza ni ngumu na hivyo amewandaa wachezaji wake kukabiliana na ushindani huo ili mwisho wa msimu wawe kwenye nafasi nzuri.

Hata hivyo, Katwila alitua Ihefu akitokea Mtibwa Sugar ambayo pia haikuwa na mwanzo mzuri wa ligi msimu huu.

Ihefu ndiyo timu inayoburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi tano tu, kati ya mechi 10 walizocheza baada ya kushinda mechi moja, sare mbili na kufungwa michezo saba.

Ihefu ilionja ushindi wa kwanza kwenye ligi hiyo Septemba 13, mwaka huu kwa kuwafunga Ruvu Shooting ya Pwani bao 1-0.

Baada ya hapo timu hiyo ilicheza mechi sita bila kupata ushindi, ikifungwa mechi zote na kutoka sare moja tu, dhidi ya Mbeya City.

Mechi nyingine za Ligi Kuu Tanzania Bara zitakazochezwa leo ni kati ya Coastal Union dhidi ya Simba ambayo itafanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha huku JKT Tanzania wakiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma watawaalika Gwambina wakati vinara wa ligi hiyo, Azam FC, watawafuata KMC kwenye Uwanja wa Uhuru.

Habari Kubwa