Kaze afunguka Biashara hachomoki

30Oct 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Kaze afunguka Biashara hachomoki
  • Kocha huyo aeleza ameandaa mfumo mpya utakaowamaliza Biashara...

​​​​​​​WAKATI kikosi cha Yanga kinatarajia kwenda kutembelea kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere leo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Cedric Kaze amesema malengo yake ni kuona timu hiyo inapata matokeo ya ushindi tu katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United itakayochezwa kesho-

Cedric Kaze.

-kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kaze, alisema kikosi chake kilichoweka kambi ya muda jijini, Mwanza, kiko tayari kwa ajili ya kuwakabili Biashara United na mikakati yake ni kuondoka na pointi tatu muhimu.

Kaze alisema anajua mechi hiyo itakuwa na ushindani kutokana na rekodi nzuri ya Biashara United wanapokuwa kwenye uwanja wa nyumbani na ubora wa kikosi cha wapinzani wao.

Mrundi huyo alisema wamefanya maandalizi mazuri na anaamini Yanga ina nafasi nzuri ya kushinda mchezo huo huku wachezaji wake wakionyesha ari na morali kubwa ya kupambana kutafuta matokeo mazuri.

"Hakuna mechi rahisi kwetu, kila mchezo ni fainali kwetu, tumejiandaa kutafuta pointi muhimu katika mechi hii ili tuendelee kujiweka katika nafasi nzuri ya kufikia malengo yetu tunayoyatarajia," alisema Kaze.

Kocha huyo alisema kila mechi anaingia tofauti kwa sababu ya mfumo wanaotumia timu pinzani na kamwe Biashara United isitarajie kuiona Yanga waliyokutana nayo msimu uliopita au iliyocheza na KMC.

"Ninafanya mabadiliko ya mfumo kulingana na mpinzani ninayekutana naye, lakini nikiwa na lengo la kutafuta pointi tatu muhimu, tunahitaji kuendelea kupata ushindi mwingine nje ya uwanja wa nyumbani. Hii itatusaidia kufikia mipango ya klabu na timu kwa ujumla," Kaze alisema.

Aliongeza ataendelea kuwakosa wachezaji watatu ambao ni majeruhi na waliachwa Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na matibabu.

"Tutamkosa Carlinhos (Carlos), ambaye anatibiwa jeraha la enka, Balama Mapinduzi ambaye tatizo lake nimelikuta pamoja na Haruna Niyonzima anayesumbuliwa na malaria, hawa hawako kwenye mipango ya mechi ya Jumamosi," aliongeza Kaze.

Hata hivyo kocha huyo alisema kwake jambo muhimu ni kupata ushindi na suala la idadi ya mabao watakayofunga halimpi presha kwa sasa.

"Kwanza ninaangalia pointi tatu, mimi sijali tunapata idadi gani ya mabao, kikubwa tupate ushindi, tunaifuata Biashara United kwa ajili ya kuvuna pointi nyingine, hautakuwa mchezo rahisi kwa kila upande, sisi tunahitaji ushindi na wenzetu pia wataingia na mipango yao, tunapambana ili kufikia malengo," alisema kocha huyo.

Kaze ataiongoza Yanga kwa mara ya tatu katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini tayari ameshinda michezo miwili tangu alipotua klabuni hapo mapema mwezi huu.

Habari Kubwa