Kaze atoa sababu Kagera kuwashika

20Feb 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Kaze atoa sababu Kagera kuwashika

HUKU akimtetea kiungo mkabaji Zawadi Mauya kuwa si kwamba alishindwa kutekeleza kile alichokitaka, Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, amesema sababu ya kushindwa kupata matokeo dhidi ya Kagera Sugar juzi, ni kutokana na wachezaji wote kutojiamini katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara.

Lakini wakati Kaze akisema hayo, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kupata pointi moja na mabao 3 mbele ya Yanga ambayo inaongoza msimamo wa ligi hiyo.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi, timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3, huku Yanga ikitokea nyuma na kusawazisha kila ilipofungwa.

Kaze alisema hawezi kumtupia lawama mchezaji mmoja kwa sababu wote hawakufanya kile alichowaelekeza dakika 45 za kipindi cha kwanza kwa kufika kwenye eneo lao huku mabeki wa pembeni nao wakiwaruhusu wapinzani wao kupiga mipira ya krosi.

“Mpira una matokeo matatu, kushinda, kushindwa na sare, ukiangalia katika mechi ya leo (juzi), wachezaji wangu hawakufanya kile ambacho niliwapa mazoezini hii ni baada ya kukosa umakini kwenye nafasi tulizotengeneza uwanjani.

“Tumeruhusu Kagera kufika kirahisi katika eneo letu, huku mabeki wa pembeni nao hawakufanya kazi yao kwa kuruhusu wapinzani wetu kutumia madhaifu yetu kupata pointi moja na mabao matatu,”alisema Kaze.

Alisema kutomwanzisha Mukoko Tonombe katika mchezo huo ni kwa sababu alihitaji kufanya mzunguko wa wachezaji wake wote kulingana na ratiba ya mechi zao kubana na kumpa muda wa kupumzika.

“Katika wiki tuna mechi tatu, lazima kuwapo kwa mzunguko hakuna mchezaji ambaye atacheza dakika 90 zote na kutakiwa kupumzika, laiti kungekuwa na ruhusa ya kufanya mabadiliko wachezaji saba, nina imani katika kipindi cha kwanza ningewapumzisha wachezaji wawili hadi watatu," alisema.

Habari Kubwa