Kaze atoa siri ya kuichapa Mtibwa

22Feb 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Kaze atoa siri ya kuichapa Mtibwa

KOCHA Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, amesema kinachombeba ndani ya kikosi hicho ni juhudi na ibada kitu ambacho kinawasaidia kupata pointi kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wakati Kaze akisema hayo, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Thiery Hitimana, amesema udhaifu katika nafasi ya beki wa kati ni sababu kubwa ya kushindwa kupata matokeo chanya katika mchezo dhidi ya Yanga juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Makocha hao walitoa kauli hizo baada ya kumalizika mechi yao kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0, matokeo hayo yakija baada ya kulazimishwa sare ya mabao 3-3 dhidi ya Kagera Sugar kwenye mechi iliyopita.

Kaze alisema aliwasoma wapinzani wao, Mtibwa Sugar pamoja na kufahamu ubora wa kocha Hitimana, hivyo aliwataka wachezaji wake kuhakikisha wanapambana na kutumia akili kusaka ushindi katika mchezo huo.

"Juhudi za wachezaji wangu na kufuata kile ninachowapa mazoezini, ndiyo chanzo cha vita ambavyo tumefanikiwa kushinda, hivyo ni mwendelezo wetu wa kutafuta mafanikio ndani ya uwanja," alisema Kaze.

Alisema alifanikiwa kupata matokeo mazuri baada ya kuwafuatilia Mtibwa Sugar kwa muda mrefu, ikiwamo kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, Zanzibar pamoja na kutumia uzoefu wake kwa kufahamu mbinu za Hitimana.

"Ni mwalimu mzuri, niliwahi kufanya naye kazi Rwanda, tulikuwa timu pinzani kama ilivyokuwa huku, kwa sababu tayari nimewasoma na kufahamu upungufu wao ndiyo maana tukafanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 na pointi tatu muhimu," alisema Kaze.

Kwa upande wa Hitimana, alisema safu ya ulinzi hasa beki ya kati ilikuwa tatizo hasa baada ya kumkosa mbadala wa Dickson Daudi ambaye amekuwa akicheza mechi nyingi zaidi bila kupumzika.

"Najua uwezo na kiwango cha beki wangu, amekuwa akicheza mechi nyingi bila kupata mapumziko, hivyo kwa mechi hii alionekana kushindwa hasa kipindi cha pili kulingana na kasi ya Yanga, sina mbadala wake imenilazimu kuendele kumtumia.

"Wachezaji wanaocheza nafasi hiyo wapo ila si wa kuwapa nafasi kwenye mechi ya presha kama hii, nitaendelea kufanyia kazi upungufu yetu," alisema Hitimana.

Habari Kubwa