Kaze: Nitafanya makubwa Yanga

16Oct 2020
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Kaze: Nitafanya makubwa Yanga
  • ***Aahidi soka la burudani, kurejesha heshima lakini auweka 'kiporo' ubingwa wa Ligi Kuu...

KOCHA mpya wa Yanga, Cedric Kaze, amewaambia mashabiki wa timu hiyo watarajie makubwa kutoka kwake, lakini Mrundi huyo akikataa kuwahakikishia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Kaze alitarajiwa kuwasili nchini jana usiku akitokea Canada ambapo alikuwa akipata mafunzo ya ukocha ya ngazi mbalimbali.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Kaze, alisema anaamini Yanga itapata mafanikio na kuwa 'tishio' endapo kutakuwa na ushirikiano mzuri kutoka kwa wachezaji, viongozi, wanachama na mashabiki wa timu hiyo.

Kaze alisema amejiandaa kukifanya kikosi cha Yanga kicheze mpira wa burudani na ushindani na anafahamu ni moja ya malengo yake kukabidhiwa mikoba ya kuifundishisha timu hiyo iliyoko kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Kocha huyo alisema anajua Yanga imesajili wachezaji wenye uwezo mkubwa kutoka mataifa mbalimbali na wanachohitaji ni kupewa mbinu mbadala za kusaka matokeo chanya katika mechi za mashindano mbalimbali watakazocheza.

"Siwahakikishii ubingwa, kitu ambacho ninawahakikishia mashabiki wa Yanga, watakuja kwenye mechi watafurahi, watatoka wanaimba na watasema kesho yake watakuja tena kuiangalia Yanga, tunaenda kufurahi," alisema Kaze.

Aliongeza bado hajasaini mkataba na Yanga, lakini ameshakamilisha mazungumzo ya kujiunga na klabu hiyo yenye makao makuu yake Mtaa wa Twiga na Jangwani.

Aliweka wazi ameshaiangalia Yanga katika mechi zake zote za msimu huu na baadhi za mwaka jana na kuona aina ya wachezaji waliopo, hivyo anafahamu mahali atakapoanzia kukijenga kikosi hicho.

"Nimeangalia mechi zote za ligi zile wamecheza, nimeangalia mechi zao za kirafiki, mechi walizocheza mwaka jana, naweza kusema nimepata mwanga wa wapi ninatakiwa kuanza, ninachowaambia Wana-Yanga, mimi na wachezaji wangu tutawapa burudani," Kaze aliongeza.

Kaze anatua nchini kuchukua mikoba iliyoachwa na Zlatko Krmpotic, ambaye alitimuliwa hivi karibuni baada ya timu hiyo kuonekana haichezi katika kiwango cha juu.

Awali Kaze ilipaswa atue nchini kuchukua mikoba ya Mbelgiji, Luc Eymael, lakini ilishindikana kwa madai ya kubanwa na matatizo ya kifamilia na hivyo Yanga ilimtangaza Zlatko aliyedumu kwa siku 37 kuwa kocha wake mpya.

Yanga ina pointi 13 baada ya kucheza mechi tano za Ligi Kuu Tanzania Bara, imeshinda mechi nne na kutoka sare moja, imefunga mabao saba imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja.

Mtihani wa kwanza wa Kaze utakuwa Oktoba 22, mwaka huu ambapo Yanga itaikaribisha Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Uhuru jijini, Dar es Salaam.

Habari Kubwa