Kaze sasa ataka majembe Yanga

24Nov 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Kaze sasa ataka majembe Yanga

HUKU akianika dhamira yake ya kutaka 'majembe' mapya kuelekea dirisha dogo la usajili mwezi ujao, Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, amesema bado ana kazi kubwa ya kutafuta njia nyingine ya kuwanoa washambuliaji ili kuweza kupambana na mabeki na hatimaye kucheka na nyavu.

Yanga ambayo kesho itaivaa Azam FC, juzi usiku ilishindwa kuvuna pointi tatu dhidi ya Namungo FC, kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Benjamini Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Kaze alisema hawajafurahishwa na matokeo hayo ambayo yamewanyima nafasi ya kuongoza ligi, lakini bado anahitaji muda wa kuwapa mbinu mpya washambuliaji wake ili kumudu kutumia vema nafasi wanazopata kwa kuvuna idadi kubwa ya mabao.

Alisema dakika 45 ya kipindi cha kwanza katika mechi yao dhidi ya Namungo walipata nafasi nyingi za wazi na kupoteza kwa sababu ya washambuliaji wake kutokuwa na purukushani za madhara kwa mabeki wa timu pinzani.

“Kulingana na jinsi safu ya ushambuliaji ilivyo, nahitaji kupata watu, ila sitaweza kuweka wazi kwa sababu nitawavunja moyo wachezaji niliokuwa nao wakati bado tuna michezo sita kabla ya dirisha la usajili kufunguliwa,” alisema Kaze.

Alisema mbali na washambuliaji wake alisema ameona mapungufu katika safu ya ulinzi kwa kutokujipanga vizuri na wakicheza bila ya maelewano, hivyo kuiruhusu Namungo kutumia udhaifu wao kusawazisha muda mfupi baada ya kupata bao.

“Tulikosa mwelekeo baada ya kushindwa kujua tunazuia kuelekea wapi, jambo ambalo limetokea kwenye mechi tatu mfululizo tulizopata sare hivi karibuni, ikiwamo dhidi ya Gwambina, Simba na Namungo, hilo nalo nimeliona naenda kulifanyia kazi,” alisema kaze.

Habari Kubwa