KCB, Rock City Marathon safi

05Aug 2021
Na Mwandishi Wetu
Mwanza
Nipashe
KCB, Rock City Marathon safi

BENKI ya KCB Tanzania imekabidhi hundi ya Sh. milioni 20 kwa waandaaji wa mbio za Rock City Marathon zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 24, mwaka huu jijini Mwanza.

Mratibu wa mbio za Rock City, Kasara Naftal (kulia) akipokea mfano wa hundi yenye thamani Sh. milioni 20, kutoka kwa Mkuu wa Masoko, Mawasiliano na Mahusiano Benki ya KCB Tanzania, Christina Manyenye, kwa ajili ya maandalizi ya mbio hizo zitakazofanyika Oktoba 24, mwaka huu Jijini Mwanza. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Akikabidhi hundi hiyo, Mkuu wa Masoko, Mawasiliano na Mahusiano wa KCB Tanzania, Christina Manyenye, alisema udhamini huo unalenga kuunga mkono jitihada za waandaji wa mbio hizo, pamoja na serikali kwa ujumla katika kuhamasisha michezo na utalii wa ndani hapa nchini.

“KCB tunafuraha kwa mara nyingine kushiriki kikamilifu kwenye mbio hizi. Tumekuwa tukiguswa sana na masuala ya kimichezo sababu tunaamini ustawi wa sekta yetu ya benki unategemea sana uimara wa wanananchi katika kujenga uchumi wao na ili hilo lifanikiwe, tunahitaji kuwa na watu wenye utimamu kiafya na kiakili. Michezo ni moja ya namna bora kabisa katika kujenga afya ya wateja wetu na kuburudika,’’ alisema Manyenye.

Alisema, ili kutangaza utalii wa ndani benki hiyo itaendelea kushirikiana na waandaaji wa mbio hizo kuhakikisha zinafanikiwa kuvutia zaidi washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, ambao ujio wao hautaishia katika kuimarisha sekta ya utalii pekee, bali utafungua milango ya mahusiano ya kibiashara kwa wakazi wa Jiji hilo.

Mratibu wa mbio hizo, Kasara Naftal aliishukuru benki hiyo kwa kuunga mkono mbio hizo.

“Ushiriki wa benki ya KCB iliyojijengea heshima kubwa kupitia huduma zake ndani na nje ya mipaka ya nchi utatusaidia pia kuvutia wadau na washiriki kutoka nje ya nchi, hatua ambayo ni muhimu katika kufanikisha agenda yetu ya kutangaza utalii wa ndani husani kanda ya Ziwa,’’ alisema Naftal.

Alisema maandalizi ya mbio hizo yanaendelea vizuri huku akibainisha kuwa ubora wa vifaa kwa ajili ya washiriki wa mbio za mwaka huu ikiwamo medali na fulana unatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa washiriki.

“Zaidi tunashukuru kuona viongozi mbalimbali wa kiserikali pamoja na wadhamini na wadau wetu wengine watashiriki kikamilifu kwenye mbio hizi.’’ alisema mratibu huyo.

Naye, Ofisa Biashara, Mahusiano ya Makampuni kutoka Tigo Pesa, Amani Chuo, alisema kampuni hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha washiriki wa mbio hizo wanajisajili kwa urahisi na kwa uhakika.

Wadhamini wengine wa mbio hizo ni pamoja na Kampuni za TIPER, Pepsi, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),Kampuni ya Uhandisi ya Magare, Unilever, NSSF, Hospitali ya Bugando, Hospitali ya CF, Garda World, Maji ya Uhai, Azam TV, Rock City Mall, Hotel Farm, EF Outdoor, The Cask na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) cha jijini Mwanza.