Kichuya, Banda watemwa Stars

13Jun 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Kichuya, Banda watemwa Stars
  • ***Makonda awaonya wanaoibeza Afcon, Amunike afunguka ubora wao wakiivaa Misri leo huku...

WAKATI timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), ikitarajia kushuka dimbani leo kuwavaa Misri katika mchezo wa kirafiki mjini Alexandria, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Emmanuel Amunike, ametangaza kuwatema nyota tisa akiwamo Shiza Kichuya na Abdi Banda.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) Wallace Karia na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (kulia), wakionyesha jezi mpya za timu ya soka ya Taifa ‘Taifa Stars’ baada ya uzinduzi uliofanywa jana jijini. Jezi ya bluu ni ya nyumbani na njano ya ugenini. MPIGAPICHA WETU

Wachezaji wengine walioachwa katika kikosi cha mwisho ni Claryo Boniphace, Selemani Salula, David Mwantika, Fred Tangalu, Miraji Athumani, Shaban Chilunda na chipukizi, Kelvin John.

Akizungumza jana baada ya kutangaza kikosi chake nchini Misri, Amunike alisema anaamini mchezo wa leo utasaidia kubaini makosa yaliyobaki kikosini na kuyafanyia kazi kabla ya kuanza kwa fainali hizo.

"Mechi hii ya kwanza dhidi ya Misri itatupa nafasi ya kuona idara tulizoimarika na zenye mapungufu, itatusaidia kujitathimini na itatuweka tayari kuanza kwa mashindano kabla ya kucheza mchezo mwingine dhidi ya Zimbabwe," alisema Amunike.

Kikosi kamili cha Stars kitakachoshiriki Afcon kinaundwa na Aishi Manula, Metacha Mnata, Aron Chalambo, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Mohammed Hussein 'Zimbwe Jr", Himid Mao, Feila Salum "Feitoto", Frank Domayo, Yahya Zayd, Aggrey Moris, Kelvin Yondani, Mudathir Yahya, Ally Mtoni, John Bocco, Thomas Ulimwengu, Farid Mussa, Simon Msuva, Rashid Mandawa, Abdillahie Mussa, Vicent Philipo, Erasto Nyoni na Mbwana Samatta.

Makonda afunguka

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amewataka wadau wa michezo nchini kuacha kuibeza Taifa Stars ambayo inatarajia kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) 2019, zinazotarajiwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19 nchini Misri.

Akizungumza katika uzinduzi rasmi wa jezi za Taifa Stars, Makonda, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya timu hiyo, alisema kufanya hivyo kunawakatisha moyo wachezaji ambao wamepewa dhamana ya kupeperusha bendera ya nchi kwenye mashindano hayo makubwa barani Afrika.

Makonda alisema huu si wakati wa kuwakatisha tamaa wachezaji wa timu hiyo na badala yake wadau wanatakiwa kuwaunga mkono ili waweze kufanya vizuri katika mashindano hayo yanayoshirikisha nchi 24.

"Tuache kuwabeza, tusiwakatishe tamaa wachezaji wetu, wametoka Simba, Yanga, Azam, Lipuli, Kagera Sugar, tuheshimu mchango wao, hiki ni kipindi cha kuonyesha mahaba kwa timu na kwa taifa, tuangalie mazuri, tuyakuze, tuache kuongea mapungufu, tuongee vitu chanya kuhusiana na timu yetu, na taifa letu," alisema Makonda.

Alisema anafahamu timu hiyo iliondoka kinyonge, lakini hilo lilitokana na ratiba iliyobana ila yeye na kamati yake wanaendelea kukusanya ahadi kutoka kwa kampuni zaidi ya 40, ambayo kila moja litatoa kiasi cha Sh. milioni 10 ili kuwahamasisha wachezaji wa timu hiyo wafanye vizuri.

Kiongozi huyo alisema kuwa ili kuonyesha mapenzi kwa Stars, amewataka mashabiki wa soka nchini kununua jezi hizo katika maduka rasmi na kuwatahadharisha wale watakaodurufu jezi hizo, watachukuliwa hatua kali.

"Ni historia mpya, jezi hizi zitaonyesha umoja wetu, mapenzi yetu kwa Stars, uzalendo wetu, itaonyesha kielelezo cha Utanzania wetu kuanzia mtaani hadi kimataifa," alisema Makonda huku pia akitangaza kununua jezi 100 na kuwapatia wajumbe wake walioshiriki katika mchakato wa kuhakikisha timu hiyo inakata tiketi ya kucheza fainali hizo za Afcon.

Habari Kubwa