Kichuya na Tambwe wote fiti kuzibeba Simba na Yanga SC

15Oct 2016
Mahmoud Zubeiry
Dar es Salaam
Nipashe
Kichuya na Tambwe wote fiti kuzibeba Simba na Yanga SC

WAFUNGAJI wa mabao katika sare ya 1-1 kwenye mchezo wa watani Oktoba 1, mwaka huu, Amissi Tambwe wa Yanga na Shizza Kichuya wa Simba wote wako fiti kuzichezea timu hizo katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wikiendi hii.

Simba SC leo watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar, wakati keshokutwa Yanga watamenyana na Azam FC katika mfululizo wa Ligi Kuu.

Kichuya aliumia kifundo cha mguu Jumatano Simba SC ikishinda 2-0 dhidi ya wenyeji, Mbeya City na kuzua hofu ya labda ataukosa mchezo wa leo – lakini Daktari wa Wekundu hao wa Msimbazi, Yassid Gembe alisema jana winga huyo mwenye kasi anaendelea vizuri.

“Kichuya anaendelea vizuri na leo (jana) jioni atafanya mazoezi. Kwa upande wangu mimi kama daktari anaweza kucheza, sasa ni uamuzi wa benchi la Ufundi tu kumpanga au akutompanga kesho (leo),”alisema Gembe.

Kichuya Jumatano aliseti bao la kwanza lililofungwa na Ibrahim Hajib kabla ya kufunga la pili Simba SC ikijiimarisha kileleni kwa ushindi wa 2-0.

Aidha, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh jana alisema kwamba tegemeo la mabao la timu yao, Tambwe anaendelea vizuri baada ya kuumia katika mchezo wa Jumatano timu hiyo ikishinda 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro Uwanja wa Uhuru.

Mrundi huyo aliumia dakika ya 87 jana baada ya kugongana na kiungo wa Mtibwa Sugar, Shaaban Nditi na kupasuka juu ya jicho, hivyo kushindwa kuendelea na mchezo.

Habari Kubwa