Kidao: Stars itafuzu Afcon

20Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kidao: Stars itafuzu Afcon
  • ***Asema tukijipanga na kufanya maandalizi bora hakuna kitakachoshindikana...

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema kuwa Timu ya Taifa (Taifa Stars), inaweza kukata tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2021), zitakazofanyika nchini Cameroon endapo tutajipanga na kujiandaa vema na michuano hiyo.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF).

Taifa Stars iliyoshiriki fainali za Afcon mwaka huu huko Misri, ilitolewa katika hatua ya makundi baada ya kufungwa mechi zote tatu ilizocheza za Kundi C dhidi ya Senegal, Kenya na Algeria.

Katika kampeni ya kuwania tiketi ya kushiriki fainali hizo zijazo, Taifa Stars imepangwa katika Kundi J pamoja na timu za Tunisia, Libya na Equatorial Guinea. Libya na Equatorial Guinea, hazikushiriki kwenye fainali za mwaka huu ambazo zilimalizika rasmi jana.

Mechi za kwanza za kuwania tiketi ya kushiriki fainali hizo zitachezwa kati ya Agosti 7 na 15 mwaka huu wakati marudiano yatakuwa ni kati ya Novemba 11 na 19 mwaka huu huku za pili zikichezwa kati ya Agosti 31 hadi Septemba 8 mwakani na marudiano yakipangwa kufanyika kati ya Oktoba 3 hadi 15 mwakani.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, alisema kuwa kundi hilo la Taifa Stars ni gumu, lakini katika dunia ya soka ya sasa hakuna timu nyepesi.

Kidao alisema kuwa mpira wa miguu sasa umebadilika na kinachotakiwa ni timu kuandaliwa vema ili iweze kupambana katika mechi zake zote za nyumbani na ugenini.

"Ni moja ya makundi magumu, lakini mpira umebadilika sana,tukijipanga vizuri kwa kufanya maandalizi mazuri, tunaamini tutafuzu," alisema Kidao, mchezaji wa zamani wa Simba na Mwenyekiti aliyejiuzulu wa Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA).

Katibu huyo alisema pia shirikisho hilo liko katika hatua za mwisho za mazungumzo na mdhamini mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Mdhamini wa ligi ameshapatikana, tupo katika hatua za mwisho za mazungumzo kabla ya kusaini mkataba," Kidao alisema katika mahojiano maalumu.

Aliongeza kuwa changamoto ya mabadiliko ya ratiba ya Ligi Kuu Bara iliyotokea mwaka jana na kusababisha kuwa na mechi nyingi za viporo, Kidao alisema kuwa ilitokana na mabadiliko yaliyofanywa katika kalenda ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambayo ilibadili mwanzo wa kuanza msimu katika mashindano yake ya Ligi ya Mabingwa na Kombe na Shirikisho.

Kuhusu sherehe za tuzo, kiongozi huyo alisema kuwa shirikisho linaendelea kufanyia kazi na zimechelewa kutolewa kwa sababu ya changamoto ya kukosa mdhamini mkuu wa ligi hiyo kwa msimu uliopita.

Habari Kubwa