Kigogo michezo ajitosa ubunge wa Kinondoni

15Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kigogo michezo ajitosa ubunge wa Kinondoni

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga na mdau mkubwa wa soka nchini, Abbas Tarimba, amejitosa kwenye mbio za ubunge baada ya jana kuchukua na kurejesha fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa na CCM kugombea Jimbo la Kinondoni.

Mwenyekiti wa zamani wa Klabu ya Yanga, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Uwekezaji wa SportPesa Tanzania, Abbas Tarimba, akizungumza na vyombo vya habari, jana, baada ya kurejesha fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa na CCM kugombea ubunge wa Jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam. NA MPIGAPICHA WETU

Milango ya kuomba kuteuliwa kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, ilifunguliwa rasmi jana na Tarimba akawa miongoni mwa waliojitokeza kuomba ridhaa hiyo kwa chama chake.

Nipashe ambalo jana lilitanda katika ofisi mbalimbali za chama hicho nchini ili kujua watiania wake, jana lilimshuhudia Tarimba akifika Makao Makuu ya CCM Mkwajuni, Kinondoni saa 2:00 asubuhi akiwa peke yake na kuingia ofisini kuchukua fomu hiyo kabla ya baadaye majira ya saa 3:00 kuirejesha.

Mara baada ya kurudisha fomu hiyo, Tarimba alisema kuwa anaamini ni muda muafaka kwake kuomba ridhaa ya chama chake kumteua kuwatumikia wakazi wa Kionondoni baada ya kujitathmini kabla ya kuchukua maamuzi ya kuchukua fomu ya kugombea.

Tarimba, ambaye ni Mkurugenzi Uwekezaji wa SportPesa Tanzania, alisema amepanga kuwatumikia vizuri Wanakinondoni kwa kuhakikisha wanapiga hatua ya kimaendeleo endapo atapata ridhaa ya chama chake na baadaye kushinda katika uchaguzi huo.

Aliongeza kuwa anafahamu changamoto zote za wilaya hiyo kutokana na kuwahi kuwa Diwani wa Kata ya Hannanasifu, Kinondoni kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia 2005 hadi 2015.

“Nina uwezo wa kikazi na dhamira ya kuwatumikia Wanakinondoni, kwani nafahamu changamoto nyingi zilizokuwapo kwenye wilaya hii, hivyo sina hofu kwani nina sifa zote za mimi kugomea hapa.

“Mimi hapa Kinondoni siyo mgeni, nipo hapa ninaishi kwa muda mrefu, hivyo ninajua kitu gani ambacho wanakitaka wakazi wa wilaya hii, kikubwa niwaahidi mengi makubwa,” alisema Tarimba.

Habari Kubwa