Kikao kizito Simba SC

13Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kikao kizito Simba SC

KAMATI ya Utendaji ya Simba SC inatarajiwa kukutana leo mjini Dar es Salaam, chini ya Rais wake, Evans Elieza Aveva kujadili ushiriki wa timu katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Rais wake, Evans Elieza Aveva.

Habari za ndani kutoka Simba ambazo Nipashe imezipata zimesema kwamba kikao hicho kitafanyika leo katika hoteli ya Serena na ajenda kuu itakuwa ni kupitia taarifa ya benchi la Ufundi juu ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kwa ujumla.

Lakini pia Kamati itajadili taarifa mbalimbali ilizozipokea kuhusu mwenendo wa timu, viongozi na wachezaji kwa ujumla hususan juu ya taarifa za hujuma.

Hiyo inafuatia kuwepo kwa taarifa za baadhi ya wachezaji kutumiwa kuihujumu timu katika mechi mbili za mwisho za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.

Simba SC ilianza vyema Ligi Kuu na kuongoza kwa muda mrefu ikicheza mechi 13 bila kupoteza, ikishinda 11 na sare mbili.

Lakini ghafla kibao kikageuka kwenye raundi mbili za mwisho na timu hiyo ikapoteza mechi mbili mfululizo, ikifungwa 1-0 African Lyon Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na 2-1 na Prisons Uwanja wa Sokoine Mbeya.

Kwa sababu hiyo, Simba SC ikamaliza mzunguko wa kwanza inaongoza kwa pointi mbili tu zaidi dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga (35-33) kutoka tofauti ya pointi nane.

Habari Kubwa