Kikwajuni yapigwa tafu

21Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR
Nipashe
Kikwajuni yapigwa tafu

TIMU ya Kiwajuni inayoshiriki Ligi Daraja la Pili, imepigwa tafu ya vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh. milioni mbili na mfanyabiashara na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini visiwani Zanzibar, Mohammed Raza.

Vifaa walivyokabidhiwa ni jezi pea 18, viatu pea 20, soksi, mipira, koni, vibendera vya waamuzi, filimbi, kadi na nyavu.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Raza alisema lengo la kutoa msaada huo ni kuisaidia timu hiyo kukabiliana na changamoto walizonazo na kuweza kufanya vizuri katika ligi yao.

Alisema timu ya Kikwajuni inahistoria kubwa katika soka la Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, hivyo hatua iliyofikia timu hiyo ipo haja ya viongozi na wapenzi wa michezo kusaidia timu pale zinapohitaji msaada wao.

Alisema vifaa hivyo vitaweza kuwasaidia wachezaji pamoja na viongozi kupunguza gharama na bajeti waliyojiwekea katika kununua vifaa vya michezo hususan vile vya mazoezi.

“Timu ya Kikwajuni ni timu kubwa hakuna asiyeijua timu ambayo katika miaka ya nyuma kwenye soka la Zanzibar iliweza kufanya vizuri,”alisema.

Kwa upande wake Katibu wa Klabu ya Kikwajuni, Ali Sheha, alisema kwa sasa uongozi wa timu ya Kikwajuni umedhamiria kufufua timu hiyo ili iweze kurejea makali yake ya awali.

Naye mwenyekit wa klabu hiyo, Burhani Himid Msoma, alimtaka Raza kuendelea kuisaidia timu hiyo ili lifikie lengo lililokusudiwa la kuhakikisha timu hiyo inarejea Ligi Kuu ya Zanzibar.

Habari Kubwa