Kili Marathon kusajili mtandaoni, Tigopesa

14Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kili Marathon kusajili mtandaoni, Tigopesa

ZIKIWA zimebaki wiki chache kuelekea katika mbio za Kilimanjaro Marathon, waandaaji wa mbio hizo maarufu ndani na nje ya nchi wamewakumbusha washiriki kujisajili mapema kwa kutumia njia ya mtandao.

Mbio za mwaka huu zinatarajiwa kufanyika Machi 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika, Moshi.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa mbio hizo, John Addison, alisema kuwa washiriki wote wanatakiwa kufuata utaratibu huo wa kujisajili kwa njia ya mtandao kwa sababu mwaka huu hakutakuwa na usajili wa kwenye vituo kama ilivyozoeleka miaka ya nyuma.

Addison alisema kuwa wameamua kubadilisha njia ya usajili na kufuata utaratibu unaofanyika katika mbio nyingine za kimataifa, ili kuwavuta washiriki wajisajili mapema na kujiepusha na usumbufu wa kukamilisha mchakato huo dakika za lala salama.

Alisema usajili ulishaanza na kila mwanariadha anayetaka kushiriki anatakiwa kujiandikisha kwa kupitia tovuti ya www.kilimanjaromarathon.com au kwa njia ya Tigo Pesa kwa kubonyeza *149*20# na hapo atapokea maelekezo.

“Kwa ambao hawana nambari za Tigo wanaweza pia kuwaomba ndugu au rafiki zao wenye namba za Tigo kuwafanyia usajili kwa kubonyeza nambari *149*20# na kisha kufuata maelekezo,” alisema mkurugenzi huyo.

Alisema ada ya ushiriki kwa wanariadha Watanzania na wakazi wa Afrika Mashariki ni Sh. 20,000 kwa mbio za kilomita 42 na nusu marathoni (kilomita 21), huku Sh. 5,000 ikiwa ni ada ya wale watakaoshiriki mbio za kilomita tano.

“Tunatoa wito kwa washiriki wote wajisajili mapema kwa kuwa usajili utafungwa idadi ikikamilika au itakapofika Februari 7 mwaka huu," Addison alisema.

Hata hivyo, alisema kutakuwa na vituo mbalimbali vya kuchukua nambari za washiriki jijini Dar es Salaam, Arusha na Moshi na kuwa washiriki watatangaziwa tarehe, sehemu na muda wa kuchukua nambari zao.

Habari Kubwa