Kili Stars yaipania  Libya Chalenji leo

03Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Kili Stars yaipania  Libya Chalenji leo

IKIWA bila ya wachezaji wake nyota wa kulipwa, timu ya soka ya Tanzania Bara "Kilimanjaro Stars" leo inatarajia kutupa karata yake ya kwanza kuwania ubingwa wa mashindano ya Kombe la Chalenji kwa kucheza dhidi ya wageni Libya mchezo utakaopigwa katika mji wa Machakos, Kenya.

Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Ammy Ninje.

Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Ammy Ninje, alisema jana katika mahojiano kuwa anakiamini kikosi chake ni imara na kitapambana kusaka matokeo mazuri ambayo Watanzania wanayasubiri.

Ninje alisema kuwa kikosi hicho kina muunganiko wa wachezaji wenye vipaji na uzoefu wa kimataifa ambao utawasaidia kukabiliana na changamoto kutoka kwa wapinzani wao.

Alisema kuwa kwao kila mechi ni fainali na hawataidharau mechi yoyote ya hatua ya makundi ambapo wao wamepangwa Kundi A pamoja na majirani Zanzibar Heroes, Rwanda (Amavubi) na wenyeji Kenya (Harambee Stars).

Naye nahodha wa Kilimanjaro Stars na beki wa Simba, Erasto Nyoni, alisema kuwa wanashukuru wamepata maandalizi mazuri na wakiwa kwenye michuano hiyo wanafikiria kutwaa ubingwa.

"Tunakwenda kushindana, tunajua hakuna mechi rahisi kwenye mashindano hayo kuanzia hatua ya kwanza, tunaahidi kuonyesha uwezo wa juu ili tupate mafanikio," alisema nahodha huyo.

Kabla ya mechi hiyo, mchana Harambee Stars wataikaribisha Amavubi na kesho kutakuwa na mechi moja ya Kundi B kati ya Burundi dhidi ya Ethiopia.

Habari Kubwa