Kili Stars, Zanzibar Heroes hapatoshi

07Dec 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe
Kili Stars, Zanzibar Heroes hapatoshi

TIMU ya soka ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), inatarajia kuwakaribisha "ndugu zao" Zanzibar (Zanzibar Heroes) katika mechi ya Kundi A ya mashindano ya Kombe la Chalenji itakayopigwa leo kwenye Uwanja wa Machakos ulioko nje kidogo ya Jiji la Nairobi.

Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Ammy Ninje

Katika mechi hiyo ambayo itaanza saa 8:00 mchana, Kilimanjaro Stars itashuka uwanjani ikiwa na pointi moja wakati Zanzibar Heroes wao wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-1 walioupata dhidi ya Rwanda (Amavubi).

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Ammy Ninje, alisema kikosi chake kiko vizuri na tayari kwa mchezo wa leo baada ya kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika mechi ya kwanza dhidi ya Libya.Ninje alisema kuwa ameiona Zanzibar Heroes na amewapanga vyema wachezaji wake jinsi watakavyowakabili wapinzani wao kwa lengo moja la kupata ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

"Tuna majeruhi mmoja (Mbaraka Yusuph), kwa kifupi kikosi changu kiko vizuri, tumeyafanyia kazi mapungufu yaliyokuwapo na bahati nzuri jana (juzi) nilipata nafasi ya kuiona Zanzibar na kuona pia mapungufu yao, siwezi kuyasema, lakini tumejiandaa vyema, nitawaweka vizuri wachezaji wangu na hatimaye tupate ushindi, " alisema Ninje.

Nahodha wa Kilimanjaro Stars, Himid Mao, aliliambia gazeti hili jana kuwa wachezaji wa timu hiyo hawana wasiwasi wowote kuhusiana na mchezo wa leo kwa sababu wanafahamiana vizuri na kikubwa wanajipanga kucheza kwa utulivu.

"Kila mmoja wetu ana hamu ya kufanya kitu fulani ili kuipa timu ushindi, tunahitaji kuwa watulivu, ni mechi ambayo huwa ya (kibabe), lakini akili yetu ikiwa makini na kuuzingatia mchezo na kujua kilichotupeleka uwanjani, tutafanya vizuri," alisema Mao.

Kocha Mkuu wa Zanzibar Heroes, Hemed Suleiman Morocco, alisema kuwa wao wanataka kuendeleza kufanya vizuri katika mashindano haya ambayo ndiyo pekee timu yao ya Taifa inashiriki.

"Kama tulivyoingia tukiwa kimya dhidi ya Rwanda na Tanzania Bara tutawakabili hivyo hivyo, tunamuomba Mungu tutimize malengo yetu," alisema Morocco.

Mechi nyingine ya Kundi A itakayochezwa leo jioni ni kati ya Rwanda dhidi ya Libya ambao ni wageni walioalikwa katika mashindano ya mwaka huu huku waalikwa wengine, Zimbabwe wakijitoa siku moja kabla ya michuano kuanza.

 

Habari Kubwa