Kim Poulsen afurahishwa na Serengeti Boys wapya

15Oct 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kim Poulsen afurahishwa na Serengeti Boys wapya

MSHAURI Mkuu wa Ufundi katika Programu za Soka ya Vijana nchini, Mdenmark Kim Poulsen amevutiwa na vijana wanaondaliwa kuwa timu mpya ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Buys.

Mdenmark Kim Poulsen.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeanza kuandaa kikosi kipya cha Serengeti Boys kitakachoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri huo mwaka 2019.

Na hiyo inafuatia kupewa uenyeji wa fainali za U-17 mwaka 2019 na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), hivyo sasa TFF imeanza kuandaa vijana wake kwa ajili ya fainali hizo za nyumbani.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas Mapunda alisema jana katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari kwamba, Kwa kuanzia tu, wanawamulika vijana 22 wanaosoma shule za Alliance zilizoko Mwanza.

Mapunda alisema mapema wiki hii, TFF ilimuagiza Mshauri Mkuu wa Maendeleo ya Vijana, Mdenmark Kim Poulsen kupima uwezo wa vijana hao kwa kufanya nao mazoezi kwenye viwanja vya Alliance hadi jana asubuhi.

“Tuna timu bora ya taifa. 2019 si tu kwamba Tanzania itashiriki, bali kushindana. Lakini naipongeza TFF na Alliance kwa kuanza programu ya kuandaa timu bora.

Serengeti Boys ya sasa inayomaliza muda wake iliandaliwa kwa mwaka mmoja, lakini vijana hawa wenye umri wa miaka 12 na 13 ni hazina nyingine kubwa kwa taifa,”alisema Poulsen.

“Kwa jinsi nilivyowaona itoshe kusema tu tayari tuna timu. Nimesikia viongozi wa TFF wakisema kwamba jicho lao si kwa vijana hawa tu, bali pia kwa vijana wengine Tanzania nzima.

Hili ni jambo zuri lenye manufaa mazuri,” alisema Poulsen alipozungumza na Waandishi wa habari jana baada ya mazoezi ya asubuhi.

Habari Kubwa