Kipre Tchetche azikana Simba, Yanga

20Nov 2016
Mahmoud Zubeiry
Nipashe Jumapili
Kipre Tchetche azikana Simba, Yanga

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Azam FC, Kipre Tchetche amesema hajazungumza na Simba wala Yanga kuhusu mpango wa usajili.

Kipre Tchetche.

Mchezaji huyo wa Al Suwaiq ya Oman, aliliambia Nipashe jana kuwa hastaajabu chochote juu ya kelele za Simba na Yanga, kwani ni kawaida yao tangu anacheza Tanzania zilikuwa zikisema zitamsajili.

“Sijazungumza na timu yoyote. Kwanza hata namba yangu ya sasa sidhani kama wanayo. Ila ni kawaida yao hao tangu nipo huko wanasema hivyo hivyo,”alisema.

Kipre alisema kwa sasa ameelekeza akili yake kwa mwajiri wake, Al Suwaiq katika Ligi Kuu ya Oman hadi atakapomaliza mkataba wake Mei mwakani. “Sifikirii kubaki huku baada ya kumaliza mkataba huu, ila sijajua nitakwenda wapi,”alisema.

Hata hivyo, Kipre amewataka Simba na Yanga waache porojo kwenye vyombo vya habari na kama kweli wanamtaka wawasiliane naye.

“Tangu nipo Tanzania magazeti yalikuwa yanaandika Kipre anakwenda Yanga au Simba, lakini sikuwahi kuzungumza na kiongozi yeyote wa hizo timu. Nimekwishawazoea hao, naona huwa wanajifurahisha, kwa sababu kama wananitaka kweli ngenitafuta,”alisema.

Kipre alijiunga na Al-Nahda Al-Buraimi ya Ligi Kuu ya Oman mapema msimu huu, lakini baada ya klabu hiyo kushindwa kulipa ada ya uhamisho dau la dola za Kimarekani 50, 000 zaidi ya Sh. milioni 100 za Tanzania, Azam FC ikamuuza Suwaiq.

Alilazimika kuhamia Al Suwaiq FC kwa mkataba wa mwaka mmoja kufuatia klabu hiyo kumalizana na Azam FC na anaendelea vizuri na maisha huko kwa sasa.

Alijiunga na Azam FC mwaka 2011 kwa pamoja na pacha wake, Kipre Michael Balou baada ya wote kung’ara katika kikosi cha Ivory Coast kilichokuja kucheza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Challenge) Dar es Salaam.

Pacha wake, Balou alitemwa Azam FC baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, kufuatia ndugu yake kuondoka mwishoni mwa msimu uliopita.

Habari Kubwa