Kirengo, Wanamaji kuvaana J'pili fainali Umoja Cup 2021

29Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Rorya
Nipashe
Kirengo, Wanamaji kuvaana J'pili fainali Umoja Cup 2021

MABINGWA watetezi wa Umoja Cup (ABEGA), Shirati Mji FC, wameaga michuano hiyo baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Wanamaji FC, kwenye mechi kali ya nusu fainali iliyopigwa juzi katika Uwanja wa Maji Sota wilayani Rorya.

Kikosi cha Kirengo FC ambacho Jumapili wiki hii kitavaana na Wanamaji FC kwenye mechi ya fainali ya Umoja CUP 2021 itakayopigwa Uwanja wa Maji Sota, Rorya. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Kwa matokeo hayo, sasa Wanamaji FC watakuwa na shughuli pevu Jumapili wiki hii kwenye mechi ya fainali watakaposhuka dimbani kuvaana na Kirengo FC ambayo Jumamosi iliyopita nayo ilipata ushindi kama huo dhidi ya Mennonite FC kwenye nusu fainali ya kwanza iliyopigwa uwanjani hapo.

Pamoja na ushindi huo kwa Wanamaji FC, pia wamelipa kisasi cha kutolewa na Shirati Mji katika hatua hiyo ya nusu fainali mwaka jana.

Alikuwa ni Zeki Uromi, aliyeizamisha Shirati Mji mapema tu katika dakika ya tisa, kwa shuti kali kutoka umbali wa takriban mita 28, bao ambalo lilidumu kwa dakika zote 90 za mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki wengi.

Katika mchezo huo, Shirati Mji, ilicheza pungufu baada ya nahodha wao, Omega Mwasi, kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kuonyesha utovu wa nidhamu kipindi cha kwanza kwa kutoa lugha zisizo na staha kwa mwamuzi.

Licha ya kutolewa nje, Omega aliendelea kuonyesha utovu wa nidhamu wakati timu zikijiandaa kwenda mapumziko baada ya chukua mpira na kisha kumbabua nao mwamuzi wa mchezo huo, Nasibu.

Kwa kadi hiyo nyekundu, sasa Omega ataukosa mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kati ya Shirati Mji na Mennonite unaotarajiwa kupigwa Uwanja wa Maji Sota Ijumaa wiki hii.

Akizungumzia utovu huo wa nidhamu ulioonyeshwa na Omega, Katibu wa Kamati ya Maadili ya Umoja Cup, Telly Micky, amesema kamati yake itakaa kesho, Jumatano kujadili matukio mawili yaliyojitokeza katika nusu fainali ya kwanza ambapo mashabiki walifanyiana fujo mpaka polisi kuingilia kati na kitendo kilichoonyeshwa na nahodha huyo wa Shirati Mji katika nusu fainali ya pili.

Katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza iliyopigwa Jumamosi, Anthony Nichola, ndiye aliifungashia virago Mennonite FC baada ya kuifungia Kirengo FC bao pekee dakika ya 64 lililodumu hadi mwisho wa mchezo.

Pamoja na mvua kubwa kunyesha, mchezo huo ulikuwa kivutio kutokana na ushindani mkali na ilimlazimu mwamuzi Francis Azaria Kembo kuusimamisha kwa dakika 20 baada ya mashabiki wa Mennonite kuanzisha vurugu dhidi ya mashabiki wa Kirengo waliokuwa wanashangilia bao hilo, hata hivyo vurugu hizo zilizimwa na askari waliokuwapo uwanjani hapo kuhakikisha usalama unakuwapo.

Michuano hiyo ya Umoja Cup, imekuwa ikidhaminiwa kwa mwaka wa tisa sasa na mdau kubwa wa soka wa Rorya, Peter Owino.

Habari Kubwa