KITENDAWILI MBIA SIMBA LEO

03Dec 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe Jumapili
KITENDAWILI MBIA SIMBA LEO
  • *** Hali bado tete, Mwakyembe aalikwa kushuhudia mabadiliko, lakini...

HISTORIA mpya huenda ikaandikwa katika mkutano mkuu wa wanachama wa Klabu ya Simba ambao wanatarajia kukutana kupitisha jina la mwekezaji (mzabuni), ambaye ameshinda maombi ya kuwekeza ndani ya klabu hiyo yenye makao yake Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Mohammed Dewji "Mo".

Hata hivyo, mjadala ambao umeanza kuitikisa klabu hiyo ni tamko la serikali baada ya kutoa maelekezo kuwa mwekezaji anatakiwa kupewa asilimia 49 na kiasi cha asilimia 51 kuwa chini ya wanachama.

Lakini mwongozo huo unapingana na makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano mkuu wa wanachama uliopita ambao uliridhia mwekezaji kupewa kiasi cha asilimia 50 na wanachama kupata sehemu iliyobakia.

Taarifa ambazo gazeti hili imezipata jana zinaeleza kuwa, viongozi wa Simba wameanza vikao vya ndani na serikali kuhakikisha mchakato huo unapitishwa kwa kupata baraka kama ilivyokubaliwa na si vinginevyo.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa endapo mkutano huo utapitisha tofauti na hivyo, tayari itakuwa imevuruga mchakato ulioendeshwa wa kupata mzabuni ambao ulizingatia kuuza hisa asilimia 50.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema kuwa maandalizi ya mkutano huo yamekamilika na wanachama wanatakiwa kufika ukumbini kuanzia saa 2:00 asubuhi ili kujiandikisha na kuhakikiwa.

Manara alisema kuwa ili kupata baraka za nchi, wanatarajia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, atahudhuria mkutano huo ambao ukimalizika kama ulivyotarajiwa, Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, itaandika historia mpya na itafungua milango kwa klabu nyingine zinazofikiria kubadilisha mfumo wa uendeshwaji.

"Kama hakutakuwa na mabadiliko, tunaamini Waziri Mwakyembe tutakuwa naye pamoja na viongozi wengine mbalimbali wanaosimamia soka nchini, tunaamini tutakamilisha mkutano wetu kwa amani, mkutano huo unaajenda moja tu," alisema Manara.

Vuguvugu la ni kiasi gani cha umiliki kinatakiwa kitolewe limechukua sura mpya baada ya mapema wiki hii Waziri Mwakyembe, kuzungumza na kituo kimoja cha radio akisema kuwa huo ndiyo mwongozo wa serikali na kamwe haitazuia mabadiliko.

Simba ilianza mchakato wa kubadilisha mfumo wa uendeshaji baada ya mfanyabiashara maarufu na mdhamini wa zamani wa klabu hiyo, Mohammed Dewji "Mo" kusema yuko tayari kutoa kiasi cha Sh. bilioni 20 kwa masharti ya kupewa asilimia 51 za hisa.