Kiungo Mo aiangukia Simba

03Mar 2018
Somoe Ng'itu
Nipashe
Kiungo Mo aiangukia Simba

KIUNGO wa Simba, Mohamed Ibrahim "Mo" ameiomba radhi klabu yake kutokana na tabia ya utovu wa nidhamu ambao ameuonyesha na kusababisha kuwa nje ya kikosi kinachombana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, imeelezwa.

Mohamed Ibrahim "Mo".

Hatua hiyo ya Mo, imekuja siku chache baada ya Kocha Mkuu wa Simba inayodhaminiwa na SportPesa, Mfaransa, Pierre Lechantre, kuwa kiungo huyo amekuwa akishindwa kuweka kipaumbele programu ya mazoezi na mara kwa mara akiomba ruhusa kwa sababu ambazo ameziita si za msingi.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah "Try Again" alisema kuwa uongozi wa klabu hiyo ulikutana na mchezaji huyo na baada ya kikao, nyota huyo aliyesajiliwa akitokea Mtibwa Sugar, aliandika barua ya kuomba radhi na kuahidi hatarudia makosa aliyokuwa anafanya.

Salim alisema kikao hicho kilizaa matunda na wanaamini kitamsaidia kurejea katika "mstari" na tayari kila mchezaji ameelezwa kuwa hakuna ambaye yuko juu ya timu. 

"Sipendi kuweka wazi kila kitu kilichozungumzwa katika kikao hicho, lakini kwa kifupi Mo ameahidi kujirekebisha na kurejea kwenye hali yake ya kawaida," alisema kiongozi huyo.

Aliongeza kuwa Simba ina kanuni na sheria zake, hivyo mchezaji anapokosea, anaadhibiwa kwa kufuata misingi hiyo iliyowekwa na ni yenye lengo la kuhakikisha nidhamu inaimarika.

 

 

Habari Kubwa