Kivumbi panga uchaguzi TFF

17Jun 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Kivumbi panga uchaguzi TFF
  • ***Mayay kutema nyongo leo, Karia, Hawa Mgesa wapeta mchujo urais, pingamizi zakaribishwa...

KIVUMBI cha kukubali matokeo ama kupinga panga la mchujo wa kuwania nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), nafasi ya urais na wajumbe wa kamati ya utendaji, kinatarajiwa kujulikana leo baada ya waliopenya na waliokatwa kutangazwa jana.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchanguzi ya TFF, Benjamin Kalume (katikati), akitangaza majina yaliyopita katika mchujo wa awali wa wagombea wa nafasi mbalimbali katika shirikisho hilo jana jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura na Mwanasheria wa shirikisho hilo, Rahimu Shabani. MPIGAPICHA WETU

Katika uchaguzi huo utakaofanyika jijini Tanga Agosti 7, mwaka huu, jumla ya wagombea wa nafasi ya urais waliochukua fomu walikuwa 10, lakini waliorudisha fomu walikuwa sita, huku waliopita katika mchujo huo wa awali wakiwa ni watatu ambao ni Hawa Mniga, Evans Mgeusa na Wallace Karia, anayetetea nafasi hiyo wakati Ally Mayay, Ally Saleh 'Alberto' na Oscar Oscar wakienguliwa.

Hata hivyo, baada ya kutangazwa kuenguliwa, Alberto, alisema hajaridhika na uamuzi huo, hivyo anasubiri kwanza majibu ya barua waliyopeleka kwa msajili wa vyama, kusimamisha mchakato hadi kanuni zipitiwe upya.

"Hatuwezi kusema lolote kwa sasa, kesho (leo) tutaenda kwa msajili wa vyama kufuatilia majibu ya barua, baada ya majibu hayo ndio nitaweka msimamo," alisema Alberto.

Kwa upande wa Mayay, alisema: "Kesho (leo), nitaweka wazi msimamo wangu kuhusu kuondolewa jina langu katika mchujo wa kuendelea na mchakato wa uchanguzi."

Awali, akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya TFF jijini Dar es Salaam jana wakati wa kutangaza matokeo hayo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya uchaguzi, Benjamin Kalume, alisema walipitia fomu zote na kufanya mchujo kwa kuzingatia kanuni za uchaguzi wa shirikisho hilo.

Alisema wagombea hao watatu wamefanikiwa kupita katika mchujo huo baada ya kukamilisha vigezo ikiwamo kupata wadhamini ambapo Karia alipata 'Endorsement' (wadhamini) 18, Hawa ambaye ni mwanamke pekee akipata wadhamini sita huku Mgeusa naye akikidhi idadi ya wadhamini ambapo kanuni inasema angalau kupata watano.

"Watatu kati ya sita waliorudisha fomu, hawakupita katika mchujo huo ni Mayay alikuwa na mdhamini mmoja tofauti na kanuni ikihitaji watano na kushindwa kukamilisha baadhi ya fomu ikiwa haikuthibitishwa vyeti kwa Kamishna wa Viapo.
"Oscar Oscar hakupata mdhamini, Ally Saleh hakuwa na mdhamini, lakini vyeti vyake naye havikupita kwa Kamishna wa Viapo, kwa sababu hizo wahawakuwa na sifa za kuendelea katika mchakato huo," alisema Kalume.

Alisema kwa upande wa wagombea nafasi ya wajumbe waliopita katika mchujo huo wanaowania nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, kwa kanda zote sita; Kanda namba moja (Dar es Salaam, Lindi, Morogoro, Mtwara na Pwani), waliochukua fomu ni saba na watatu wamefanikiwa kupita katika mchujo kwa kukidhi vigezo ambao ni Athuman Kambi, Lameck Nyambaya na Hosseah Lugano.

Walioenguliwa kwa maelezo ya kutokidhi vigezo ni Ellisony Mweladzi, Jimmy Shomari, Liston Katabazi na Saady Khimji ambaye alipata mdhamini kupitia klabu ya Yanga wakati anatakiwa mdhamini wake kutoka ngazi ya mkoa.

Kalume alisema Kanda namba mbili (Mkoa wa Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga) walikuwa watatu na waliopita ni Khalifa Abdallah na Zakayo Mjema huku Thabiti Kandoro akiondolewa kwa sababu hajakidhi vigezo ikiwamo kupata mdhamini wa klabu na si mkoa.

"Kanda namba tatu (Mkoa wa Iring, Mbeya, Njombe, Ruvuma na Songwe, waliopita ni Abousufian Sillia, James Mhagama na Mohammed Mashango, ambao hawakupita ni Ulisaja Elias, Denis Manungu na Joseph Ngunangwa ambao hawakukidhi vigezo.

"Waliopita kwa Kanda namba nne (Mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Simiyu na Singida) ni Hamis Kitila, Mohammed Aden na Osuri Kosuri huku Mrisho Ramadhani akiondolewa katika mchujo huo kutokana na kutokidhi vigezo," alisema.

Aidha, Kalume alitaja wagombea watatu wote wamepita kwa upande wa Kanda namba tano (Mikoa ya Geita, Kagera, Mara na Mwanza ambao ni Salum Chama, Vedastus Lufano na Salum Alli huku kwa Kanda namba sita nao pia kipita wote watatu ambao ni Blassy Kiondo, Issa Mrisho na Kenneth Pesambili.

"Baada ya mchakato huu sasa tunaenda kwenye hatua ya kuweka na kuwekewa pingamizi kwa waliopita katika mchakato huo na zoezi hilo linaanza Juni 19 hadi 21, baada ya hapo Juni 22 hadi 24 kusikiliza pingamiza hizo na Juni 25 hadi 27 tutakuwa na zoezi la usahili," alisema makamu mwenyekiti huyo.

Habari Kubwa