Kiwango cha Manula chamvuruga Makonda

01Jun 2019
Somoe Ng'itu
DAR
Nipashe
Kiwango cha Manula chamvuruga Makonda

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema kuwa kiwango kilichoonyeshwa na kipa wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Aishi Manula, katika mechi ya marudiano ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe alicheza kwa kiwango cha juu.

 

 

 

Katika mechi hiyo iliyochezwa mjini Lubumbashi, Simba ilifungwa mabao 4-1 na kutolewa katika mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Awali Makonda alitangaza kumpatia zawadi ya Sh. milioni tano kipa huyo wa zamani wa Azam FC, lakini jana kiongozi huyo alisema sasa atampa zawadi ya Sh. milioni 10.

Akizungumza katika sherehe za Tuzo za Mo 2019 zilizofanyika juzi jijini Dar es Salaam, Makonda alisema kuwa kila akikumbuka kiwango kilichoonyeshwa na Manula katika mechi hiyo ya ugenini, akili yake ‘inavugugika sana.’

"Golikipa wetu katika ile mechi iliyochezwa kule Congo, alifanya kazi kubwa sana, akishirikiana na wenzake, nimefikiri, Jumatatu saa 4:00 asubuhi, kila anayepata tuzo hapa ataambana na golikipa, aliivuruga sana akili yangu, " alisema Makonda.

Aliongeza kuwa kila siku akiifikiria ile mechi, anajisikia furaha sana.

"Wale wengine wote wataambana na golikipa wetu, golikipa atapata milioni 10, halafu wenzake watapata Sh. milioni moja moja, jumla itakuwa Sh. milioni 20, alifanya kazi kubwa sana, akishirikiana sana na wenzake,"

Manula alitangazwa kuwa Kipa Bora wa Mwaka wa Simba kwa msimu wa pili mfululizo wake tuzo ya Mchezaji Bora ikienda kwa Mnyarwanda Meddie Kagere aliyefunga mabao 23 katika Ligi Kuu Tanzania Bara pia alishinda tuzo ya Mfungaji Bora.

Mchezaji mwingine aliyeng'ara katika tuzo hizo alikuwa ni Erasto Nyoni ambaye alishinda Tuzo ya Beki Bora na Tuzo ya Wachezaji wakati Mzambia Clatous Chama alishinda Tuzo ya Goli Bora, James Kotei (Kiungo Bora), John Bocco (Mshambuliaji Bora), Rashid Juma (Mchezaji Bora Chipukizi) na Mwanahamisi Omary wa Simba Queens aliibuka mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora Mwanamke.

Mfadhili wa zamani wa klabu hiyo, Azim Dewji alitangazwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Heshima na baada ya kupokea tuzo hiyo alimtaja Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, ndiye aliyemshauri kuwekeza katika klabu ili kuwaandaa wachezaji kwa ajili ya kuitumikia Timu ya Taifa (Taifa Stars).

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed Dewji (MO), aliwaambia washindi wa tuzo hizo wanatakiwa kuongeza juhudi ili mwakani wafanye vema zaidi na kuwataka wale ambao hawajashinda wasione kama wao ni wabovu na badala yake kuendelea kujituma.

Habari Kubwa