Kiwango cha Mwakinyo, Zarika gumzo England

21Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kiwango cha Mwakinyo, Zarika gumzo England

BONDIA nyota Mtanzania, Hassan Mwakinyo amewasili jijini, Nairobi Kenya salama na yuko tayari kwa pambano lake la kimataida dhidi ya Eduardo Gonzalez kutoka Argentina lililopangwa kufanyika keshokutwa kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta, imefahamika.

Bondia Mtanzania, Hassan Mwakinyo, akiwasili jijini Nairobi Kenya, akitokea kambini England, alipokuwa akijiandaa kwa ajili ya pambano lake dhidi ya Eduardo Gonzalez kutoka Argentina litakalofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta keshokutwa. PICHA: SPORTPESA

Mwakinyo kwa sasa ananoa makali yake chini ya kocha, Tony Bellew, kutoka Liverpool, England ambako alikuwa kambini chini ya ufadhili wa Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya SportPesa.

Mbali ya Mwakinyo, pia Bellew anamfundisha bondia mwanamke, Fatuma Zarika ambaye atapambana na Catherine Phiri wa Zambia katika pambano la ubingwa wa dunia wa uzito wa Super Bantamweight ambao unatambuliwa na Baraza la Ngumi za Kulipwa Duniani (WBC).

Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa Kampuni ya SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas, alisema jana kuwa Mwakinyo anafanya mazoezi chini ya uwezeshaji wa kampuni yao.

Tarimba alisema kuwa mbali ya kampuni yao kuwezesha kambi ya Mwakinyo na Zarika, pia Bellew amevutiwa sana na viwango vya mabondia hao na wanaamini kuwa watafanya vizuri katika mapambano yao.

Alisema kuwa mabondia hao wamepata mafunzo bora na ya kisasa kutokana na umuhimu wa pambano hilo.

“Wakiwa mjini Liverpool, Mwakinyo na Zarika walijiandaa vyema kwa kuwa wanajua ugumu wa mapambano yao. Kampuni ya SportPesa imeona umuhimu huo na lengo letu kubwa ni kuona mabondia hao wanapata matokeo mazuri na kuwafurahisha wadau wa ngumi za kulipwa katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Tarimba.

Alisema kuwa Gonzalez alitarajiwa kuwasili Kenya leo na kesho Ijumaa mabondia wote hao watapima uzito kwenye Hoteli ya The Stanley.

Pia mabondia hao watatembelea ofisi za SportPesa na kufanya mahojiano kwenye vituo mbalimbali vya televisheni na redio mbali ya kula chakula cha jioni na wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Habari Kubwa