Kiwango Simba chamkera Pablo

03Dec 2021
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kiwango Simba chamkera Pablo
  • ***Aahidi mabadiliko wakiifuata Red Arrows, FCC yaishika GSM...

LICHA ya kupata ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya Geita Gold FC, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco amesema hajaridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake na wakiendelea hivyo, watapata shida katika mchezo wao wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows ya Zambia.

Kiungo wa Simba, Jonas Mkude (kushoto), akiwania mpira dhidi ya mshambuliaji wa Geita Gold FC, Danny Lyanga katika mechi ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam juzi usiku. Simba ilishinda mabao 2-1. PICHA: SIMBA SC

Simba, wawakilishi pekee wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa watashuka ugenini keshokutwa kuwakabili Red Arrows huku wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0, waliopata Jumapili iliyopita hapa nyumbani.

Pablo alisema kitu pekee alichokipenda katika mchezo huo wa juzi ni kitendo cha kuvuna pointi tatu lakini hajaridhishwa na kiwango walichokionyesha wachezaji wake.

"Hatukuwa bora, tumecheza mchezo mbovu licha ya kushinda, tumeshindwa kutawala mpira na kuwafanya wapinzani watawale mpira, tulitengeneza nafasi na kushindwa kuzitumia, tunaenda Zambia, kwa mwendo huu basi tutakuwa na shida sana, suala la mabadiliko ya kikosi sio sababu," alisema Pablo.

Kocha huyo aliongeza atakwenda kufanyia kazi mapungufu hayo ili kuhakikisha kila mchezaji anafanya vyema majukumu yake kwa ajili ya michezo miwili iliyopo mbele yao ikiwamo dhidi ya JKT Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah 'Try Again' alisema wamejipanga vizuri kuelekea mchezo huo dhidi ya Red Arrows na kuhusu suala la 'fitna na mchezo mchafu' pia watapambana nalo.

"Mikakati yetu ni siri kubwa, mashabiki watambue timu yetu ni imara na wachezaji wanatakiwa kufanya majukumu yao, suala la nje ya uwanja ikiwamo fitna hatuna mashaka na hilo kwa sababu tuna uzoefu mkubwa katika michuano ya kimataifa," alisema kiongozi huyo.

Aliongeza kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kinatarajia kuondoka nchini leo kuelekea Zambia ambapo mshindi wa jumla wa mechi hiyo atatinga hatua za makundi.

Aliongeza hawezi kuweka wazi mikakati yao, lakini tayari benchi la ufundi na wachezaji wao wameshajipanga kuhakikisha wanapata ushindi ugenini na hatimaye wanasonga mbele katika michuano hiyo.

Wakati huo huo, kiungo mshambuliaji wa Simba, Bernard Morrison ameteuliwa kuwa Mchezaji Bora wa mashabiki wa Novemba akiwashinda Meddie Kagere na Jonas Mkude.

Kutokana na ushindi huo, Morrison ambaye kwa Novemba alicheza dakika 235 na kufunga mabao mawili na kutoa pasi za mwisho mbili, alikabidhiwa kitita cha Sh. milioni 2 na wadhamini wa tuzo hizo, kampuni ya Emirate Aluminum ACP.
Katika hatua nyingine, Tume ya Taifa ya Ushindani (FCC), imepokea malalamiko kuhusu kampuni ya GSM, kudhamini Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Urio, alisema tume hiyo italitolea ufafanuzi suala hilo baada ya kupitia vielelezo muhimu kuhusiana na mkataba huo ambao GSM wameingia na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Urio alisema FCC ilipokea malalamiko hayo Jumatatu na barua ilieleza GSM itadhamini vipi ligi hiyo huku pia ni wadhamini wakuu wa Yanga.

“Jumatatu tulipokea malalamiko ya kujua kama kitendo hicho hakitaathiri ushindani wa Ligi Kuu. Hilo siwezi kulisema kwa sasa kwa sababu tumeanza kulifanyia kazi na baada ya kulipitia kwa kina tutalitolea taarifa rasmi,” alisema Mkurugenzi huyo.

Alisema suala hilo sio la kushtukiza na wao ni kama mahakama, hivyo wanasikiliza malalamiko na kuyafanyia kazi kikamilifu.

“Mimi binafsi sijaona huo mkataba unasemaje zaidi niliona tu picha kwenye mitandao, tutaomba mkataba walioingia tuuone unasemaje,” aliongeza Urio.

Imeandikwa Saada Akida na Mary Geofrey

Habari Kubwa