Kiwango Yanga chawakuna wadau

22Apr 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Kiwango Yanga chawakuna wadau
  • ***Pamoja na kutupa nje Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Ahly ya Misri, lakini kiwango kilichoonyeshwa na wawakilishi hao wa Tanzania kimewakuna wengi...

KAMA kwenye mchezo wa soka kuna suala la bahati, basi itoshe kusema Yanga hawakuwa na bahati Misri, kwa mujibu wa wadau wa soka waliotoa maoni yao jana baada ya wawakilkishi hao wa Tanzania kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Ahly juzi usiku mjini Alexandria, Misri.

Yanga imeaga michuano hiyo kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kufungwa 2-1 kwenye mechi ya marudiano juzi usiku kwenye Uwanja wa Borg El Arab.

Wawakilishi hao wa Tanzania, walipoteza nafasi ya kusonga mbele hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kufungwa bao la 'usiku' - sekunde kadhaa kabla filimbi ya mwisho ndani ya muda wa nyongeza baada ya kumalizika dakika 90.

Akizungumzia mechi hiyo, kocha wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa, alisema kilichoiponza Yanga ni kujisahau dakika za mwisho kwa kupoteza muda.

Mkwasa aliyewahi kuifundisha Yanga, alisema kama Yanga wasingetumia mtindo wa kushambulia kwa kushtukiza kama walivyokuw wakifanya wapinzani wao, huenda matokeo yasingekuwa waliyokutana nayo.

"Hata hivyo, alisema timu hiyo haikuwa na bahati kwenye mchezo huo. "Naamini, kama watafanya marekebisho na kucheza kwa kasi, wana nafasi kubwa ya kucheza hatua ya nane bora Kombe la Shirikisho," alisema Mkwasa.

Kocha wa Mwadui, Jamhuri Kihwelu 'Julio' aliipongeza Yanga kwa mchezo mzuri na ushindani mkubwa pamoja na kupoteza mechi.

"Tangu nimeifahamu Yanga, sijawahi kuiona ikicheza soka la ushindani na maarifa makubwa kama walivyocheza juzi," alisema Julio na kuongeza:

"Walitumia nguvu na nidhamu ya kiufundi. Ilicheza kama zichezavyo timu za Ghana au Ivory Coast. Hata hivyo hawakuwa na bahati."

Alisema kama watacheza kwa kasi hiyo, wana nafasi nzuri ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.

"Walijituma sana, jambo ambalo wadau wa soka hatukulitarajia, tulidhani kule wanakwenda kufungwa mabao matano au sita," alisema Kenny Mwaisabula, mchambuzi wa soka na kocha wa zamani wa timu hiyo.

Mwaisabula alisema kama timu hiyo itaendelea kucheza kwa kiwango ilichoonyesha Misri, ina nafasi ya kufika mbali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.

"Walidhihirisha kuwa wanaweza kujituma, mpira ndiyo kazi yao, wanatakiwa kufanya hivyo katika kila mechi, lakini utashangaa jinsi watakavyocheza na Coastal Jumapili, wanaweza hata kufungwa tena, " alisema Mwaisabula.

Alimtaja kiungo wa kimataifa wa Yanga kutoka Zimbabwe, Thabani Kamusoko kuwa ndiye aliyeonyesha kiwango cha juu zaidi katika mchezo huo.

Kikosi cha Yanga kilichoko chini ya Mdachi, Hans van der Pluijm kinatarajiwa kurejea nchini leo mchana kwa maandalizi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Coastal Union Jumapili wiki hii kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Habari Kubwa