Kocha DRC awamwagia sifa Samatta na Msuva

28Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kocha DRC awamwagia sifa Samatta na Msuva

WAKATI Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Florent Ibenge, ametoa sifa kwa wapinzani wao Taifa Stars kwa kuonyesha mchezo mzuri huku akikiri Mbwana Samatta na Simon Msuva ni wachezaji wa kimataifa.

Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Florent Ibenge.

Akizungumza baada ya mechi ya kirafiki ambayo timu yake ililala mabao 2-0, Ibenge, alisema kuwa Stars walionyesha mpira wa kiufundi kipindi chote huku nyota hao wanaocheza nje ya nchi wakipambana kuisaidia timu yao kupata mabao.

Ibenge alisema kuwa makosa yaliyofanywa na safu ya ulinzi ya timu yake yaliwaruhusu washambuliaji wa Stars kufanya mashambulizi mara kwa mara kwenye lao na hatimaye kufanikiwa kupata mabao mawili.

"Nawapongeza Taifa Stars kwa kuonyesha soka la kiwango cha juu. walicheza mpira mzuri, sisi pia hatukuwa wabaya tulikosa msukumo, tunawapongeza Taifa Stars walicheza mpira wa mashambulizi na wana washambuliaji wenye kasi na wazuri ambao Samatta na Msuva, Stars ni timu nzuri",  alisema Ibenge.

Aliongeza kuwa wachezaji wake walipoteza umakini na kukiri safu yake ya kati pia ilikosa mawasiliano mazuri na kusababisha mipira kupotea ovyo.

 "Tulitaka sana tushinde huu mchezo lakini hatukuweza kuutumia mfumo tulioutarajia, tulipoteza mipira mingi katikati na kuwapa wapinzani wetu mipira, safu ya ulinzi haikusaidia kuzuia vyema mashambulizi," Ibenge alisema. 

Stars inayonolewa na Salum Mayanga anayesaidiana na Hemed Morocco imepata ushindi huo ikiwa ni siku chache baada ya kupata kichapo cha mabao 4-1 katika mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Algeria.

  

Habari Kubwa