Kocha atoa msimamo kipa Serengeti Boys

16Apr 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Kocha atoa msimamo kipa Serengeti Boys

LICHA ya kuonyesha uwezo mdogo, Kocha Mkuu wa Timu ya Soka ya Vijana ya umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), Oscar Mirambo, amesema ataendelea kumtumia kipa Mwinyi Yahya, katika mechi ya pili ya mashindano ya Afrika (Afcon U-17).

Serengeti Boys ilikubali kichapo cha mabao 5-4 kutoka kwa yosso wenzao wa Nigeria katika mechi ya ufunguzi, lakini ilionekana mabao mawili kati ya hayo yaliyofungwa yalitokana na makosa binafsi ya Mwinyi.

Wenyeji hao wa fainali hizo zinazofanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini, Serengeti Boys watashuka tena uwanjani kesho kuwakabili Uganda kuanzia saa 1: 00 usiku wakati mapema saa 10:00 katika Kundi A, Angola watavaana na Nigeria.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mirambo, alisema kufanya uamuzi wa kumbadilisha golikipa hautakuwa wa kujenga na kitakachofanyika ni kurekebisha makosa yaliyojitokeza na hapo ndio watakuwa wamefanikiwa 'kutibu tatizo'.

Mirambo alisema mechi hiyo ilikuwa ni ngumu na kitendo cha kufanikiwa kupata mabao mawili ya haraka baada ya kuanza kwa kipindi cha pili ni cha kujivunia, kwa sababu ilionekana wachezaji wake wameelewa mawaidha waliyopewa wakati wa mapumziko.

"Nafasi bado ipo, tumemaliza mechi ya Nigeria, tuna michezo miwili mkononi, tutaimarisha nidhamu mchezoni, tunajifunza kutokana na makosa, ni wazi kuwa suala la golikipa ni changamoto," alisema kocha huyo.

Leo ni mapumziko na mechi nyingine za fainali hizo za Kundi B zitachezwa keshokutwa kwa Cameroon kuwakabili Morocco wakati Senegal watawavaa Guinea kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa