Kocha Azam alia na wachezaji kujiamini sana kwa Mbao FC

08Nov 2016
Faustine Feliciane
Nipashe
Kocha Azam alia na wachezaji kujiamini sana kwa Mbao FC

KOCHA wa Azam FC, Zeben Hernandez, amesema timu yake ilijiamini sana wakati wakichezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza juzi.

Hernandez, aliiambia tovuti ya klabu hiyo kuwa wachezaji wake walijiamini sana na kujikuta wakifanya makosa yaliyowagharimu kwenye mchezo huo.

"Wachezaji wangu walijiamini sana kwenye mchezo ule kuliko wapinzani wetu na kujikuta tukishindwa kucheza katika kiwango kilichotarajiwa," alisema Hernandez.

Aidha, Hernandez alitetea mfumo wake wa 3-5-2 alioutumia kwenye mchezo wa juzi.

"Kufungwa kwetu hakukutokana na mfumo wetu, suala lipo ndani ya wachezaji wetu na maamuzi mabaya ya waamuzi wa ligi," alisema Hernandez.

Hernandez alimtupia lawama mwamuzi wa kati wa mchezo huo, Jacob Adongo kutoka Mara kwa kulikubali bao la kwanza la Mbao FC wakati mfungaji Venance Ludovick akiwa ameotea.

Matokeo hayo yameifanya Azam FC kubaki na pointi zake 22 na kushuka kwa nafasi moja hadi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, huku Kagera Sugar waliopata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ruvu Shooting wakipanda mpaka nafasi ya tatu wakiwa na pointi 24.

Kikosi cha Azam kiliondoka jana asubuhi jijini Mwanza kuelekea Shinyanga kwa ajili ya mchezo wao wa mwisho wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Mwadui FC utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Kambarage.

Habari Kubwa