Kocha Gendarmarie  aishangaa Simba SC

13Feb 2018
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kocha Gendarmarie  aishangaa Simba SC

USISHANGAE! Kocha wa Gendarmarie ya Djibouti, Issa Mvuyekure,  ameshangaa kuona kikosi chake kimefungwa mabao mchache na vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, matokeo ambayo hakutarajia wakati anatua nchini kucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha wa Gendarmarie ya Djibouti, Issa Mvuyekure.

Simba ikiwa mwenyeji katika mechi hiyo ya kwanza ya hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho ilipata ushindi wa mabao 4-0 na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo inayofanyika kila mwaka barani Afrika.

Mvuyekure alisema kuwa amekipongeza kikosi chake kwa kupambana na hatimaye kuwabana Simba na kupunguza idadi ya mabao ya kufungwa.

"Nilikuwa nafikiria Simba itatufunga magoli kuanzia 9 au 10 ndiyo tulikuwa tumezoea hivyo, Lakini sasa zimeteremka hadi kufikia nne, Alhamdulillah, naona kuwa mwakani tutakuwa sehemu nzuri zaidi,' alisema kocha huyo raia wa Burundi.

Aliongeza kuwa timu yake imeshindwa kuonyesha kandanda la kuvutia kwa sababu ya kukosa mechi za ushindani za ligi yao ambayo imemalizika tangu Desemba mwaka jana na amekuwa na kikosi hicho kwa muda wa mwaka mmoja.

Timu hizo mbili zinatarajiwa kurudiana ifikapo Februari 21 mwaka huu na mshindi atakutana kati ya El Masry ya Misri au Green Buffaloes ya Zambia.

 

Habari Kubwa