Kocha Jamhuri afafanua Yanga ilipowazidi nguvu

09Jan 2020
Isaac Kijoti
Zanzibar
Nipashe
Kocha Jamhuri afafanua Yanga ilipowazidi nguvu

LICHA ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Yanga, Kocha wa Jamhuri, Mustafa Hassan maarufu 'Mu', amesema mfumo walioutumia katika mchezo huo wa Kombe la Mapinduzi, umewaepushia balaa la kufungwa mabao mengi.

Yanga juzi usiku ilitinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi baaada ya kuibuka na ushindi huo katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan.

Mabao ya Yanga katika mechi hiyo yalifungwa na Adeyum Saleh dakika ya 45 na mtokea benchi, Mohamed Isssa 'Banka' dakika ya 85.

Kwa matokeo hayo sasa Yanga itakutana na Mtibwa Sugar leo saa 2:15 usiku katika mchezo wa nusu fainali utakaopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Unguja.

Akizungumza na Nipashe baada ya mechi hiyo, Mu alisema kwa sasa Yanga imeimarika sana katika eneo la kiungo cha kati na ndiyo idara iliyowapa sana tabu.

Alisema kama wangecheza mchezo wa wazi 'wangepigwa' mabao mengi zaidi kutokana na ubora mkubwa wa wapinzani wao.

"Kila Yanga ilipofanya 'sub' (mabadiliko) hali ilizidi kuwa mbaya zaidi kwetu na kama tungecheza 'free game', tungepigwa mabao mengi," alisema.

Aidha, alisema kitendo cha wachezaji wake kucheza na jukwaa ni moja ya tatizo lililoigharimu timu yao na kuchangia kipigo hicho juzi.

Fainali za mashindano hayo yanayofanyika kila mwaka inatarajiwa kuchezwa Januari 13, mwaka huu kwa bingwa kuondoka na kitita cha Sh. milioni 15.

Habari Kubwa