Kocha KVZ: Simba kwa kumiliki mpira kiboko

05Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Kocha KVZ: Simba kwa kumiliki mpira kiboko

KOCHA wa KVZ ya Zanzibar inayoshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, Abdulghani Msoma, ameisifia timu ya Simba kuwa inauwezo mkubwa wa kumiliki mpira zaidi ya timu nyingine zinazoshiriki michuano hiyo.

Akizungumza juzi usiku baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Simba ambao walifungwa bao 1-0, Msoma, alisema kikosi cha Simba kina wachezaji wenye uwezo mkubwa na walifanya kazi ya ziada kuwazuia wasiwafunge mabao mengi.

Alisema katika mchezo huo wa juzi, alitumia mfumo wa kushambulia ili kuwapunguza kasi wachezaji wa Simba na kupunguza umiliki wao wa mpira.

"Tumefungwa, lakini timu yangu imecheza vizuri kwa kuwabana Simba ambao kwa kweli wana timu nzuri na yenye mbinu," alisema Msoma.

Aidha, alisema kama wangeamua kucheza mtindo wa 'kupaki basi' ana uhakika wangefungwa mabao mengi katika mchezo huo.

"Kama tungecheza kwa kuzuia muda wote na kwa sababu Simba wana mbinu na wachezaji wenye uzoefu, pengine yangetukuta yale yaliyowakuta ndugu zetu wa Jamhuri ambao walijikuta wakifungwa mabao 6-0 na Yanga," alisema Msoma.

Aidha, aliweka wazi hana matumaini ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo na michezo iliyobakia kwake ataitumia kulinda heshima ya timu yake.

KVZ imejikuta ikipoteza michezo miwili mfululizo baada ya awali kufungwa mabao 2-0 na URA ya Uganda kabla ya juzi kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Simba

Habari Kubwa