Kocha Mayanja aishukia TFF

21Mar 2016
Nipashe
Kocha Mayanja aishukia TFF

KOCHA wa Simba, Jackson Mayanja, ameishukia TFF kutokana na kitendo cha shirikisho hilo la soka nchini kuzipiga kalenda mechi za Azam FC na Yanga bila sababu za msingi.

MAYANJA

Simba kwa sasa iko kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 57, saba mbele ya Yanga na Azam FC zinazoshika nafasi ya pili na ya tatu, lakini timu hiyo ya Msimbazi imecheza mechi tatu zaidi.

Na Mayanja anaona kitendo cha kuwa mechi tatu mbele ya wapinzani wake katika mbio za ubingwa msimu huu ni kukiuka taratibu za uendeshaji wa soka.

"Utaratibu huu nimeukuta Tanzania tu, tumeona timu inacheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na inacheza pia mechi zake za ligi ya nyumbani," alisema. "Lakini hapa (Tanzania) timu inaacha kucheza mechi za ligi ya nyumbani eti kisa inacheza mechi za Afrika.

"Kilichonishangaza zaidi, jana (juzi) kulikuwa na mechi za Afrika (Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho), lakini kulikuwa na mechi za ligi ya Tanzania. Si sahihi kufanya hivi. Mabadiliko yanapaswa kufanyika.

"Simba sasa tumecheza mechi tatu zaidi ya Azam na Yanga. Na wote wanapigania ubingwa. Utaratibu huu wa kusimamisha mechi zao unawapa nafasi ya kucheza huku wakiangalia matokeo yetu."

Kikosi cha Simba kiliondoka jijini hapa jana asubuhi kurejea Dar es Salaam, huku Mayanja akitoa mapumziko ya siku nne kwa nyota wake.

'COASTAL ILIKATA PUMZI'

Katika hatua nyingine, Mganda huyo alisema kikosi chake kiliizidi uwezo timu ya Coastal Union katika mechi yao ya juzi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa.

"Kila mechi ninaichukulia kama inavyokuja. Sitegemei mchezaji mmoja na 'tactics' (mbinu) zangu zinageuka kila muda," alisema. "Uliona jana (juzi nilimwanzisha Danny (Lyanga) ambaye kila mara haanzi, nikamweka (Ibrahim) Ajibu nje. (Ajibu) hakuwa na tatizo lolote, lakini ilikuwa mechi ya mbinu kali," alisema.

Ally Jangalu, kocha wa Coastal Union, alikiri timu yake kuzidiwa uwezo na mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara.
"Goli la kwanza kipa (Fikirini Bakari) alitoka kivivu, akashindwa kuuondoa mpira. Ilivyoonekana wapinzani wetu (Simba) walikuwa wazuri kuliko sisi."

Hata hivyo, kocha huyo alidai kuwa Coastal Union hawataporomoka daraja licha ya mabingwa hao wa Tanzanua Bara 1988 kukusanya pointi 19 tu katika mechi 24 zilizopita walizofungwa mabao 30, huku wakifunga 14.

"Timu yangu haikucheza vizuri. Imebaki michezo sita, hatuwezi kukata tamaa. Tukishinda mitatu, tunaweza kuwa mahali salama," alisema Jangalu ambaye kikosi chake kimefanikiwa kushinda mechi nne tu hadi sasa, mbili dhidi ya Yanga na Azam FC.

Mabao ya vichwa ya washambuliaji Lyanga na Kiiza katika kila kipindi yaliandikisha kipigo cha 13 Ligi Kuu msimu huu. Wawili hao pia waliufanya msimu kuwa idadi ya mabao kuwa 377 (kabla ya mechi ya jana ya African Sports dhidi ya Tanzania Prisons).

Habari Kubwa