Kocha mpya Yanga kuwakosa Waarabu

02May 2018
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kocha mpya Yanga kuwakosa Waarabu
  • ***Viongozi watoa sababu, kikosi kuondoka kesho kuelekea Algeria huku...

WAKATI kikosi cha wachezaji 20 na viongozi 10 wa Yanga, wakitarajia kuondoka nchini kesho kuelekea Algeria, tayari kwa mchezo wao wa kwanza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger,

Kocha mpya wa timu hiyo, Mkongoman Mwinyi Zahera.

Kocha mpya wa timu hiyo, Mkongoman Mwinyi Zahera bado anahangaikia vibali vya kufanya kazi nchini.

Hatma ya kocha huyo kama ataongozana na timu kuelekea Algeria ama la, itafahamika leo endapo viongozi watakuwa wamefanikiwa kukamilisha vibali hivyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema mpaka kufikia jana hakukuwa na taarifa za kukamilika kwa vibali hivyo.

"Tunaondoka hapa Alhamisi na wachezaji 20 na viongozi 10, lakini kwa kweli sina uhakika kama kocha wetu mpya tutakuwa naye," alisema Saleh.

Alisema timu inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza katika hatua ya makundi.

"Benchi la ufundi limefanyia kazi mapungufu waliyoyaona kwenye michezo iliyopita ukiwemo mechi  ya Jumapili iliyopita dhidi ya Simba," alisema.

Yawatema Tambwe, Kakolanya

Saleh, alisema katika msafara wa wachezaji watakaondoka kesho, hawatakuwa na washambuliaji Amissi Tambwe, Donald Ngoma na kipa Benno Kakolanya ambao bado hawajawa fiti.

"Hao ndio wachezaji ambao nina uhakika hawatakuwapo kwenye safari, ila wengine waliobaki wapo katika hali nzuri na hakuna majeruhi wengine," alisema Saleh.

Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, itacheza na USM Alger Jumapili usiku  na itarejea Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa pili dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda Mei 16, mwaka huu.

Baada ya mchezo huo, itasubiri mpaka Julai 18, mwaka huu kucheza mechi yake ya mwisho ya mzunguko wa kwanza hatua ya makundi dhidi ya Gor Mahia ya Kenya ugenini.

 

 

Habari Kubwa