Kocha Ndanda alia corona kuwatibulia

26Mar 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Kocha Ndanda alia corona kuwatibulia

KOCHA Mkuu wa Ndanda FC ya mkoani Mtwara, Abdul Mingange, amesema uamuzi wa kusimamishwa kwa Ligi Kuu Bara umemweka katika 'presha ya juu' kwa sababu umewaondoa wachezaji wake katika kasi ambayo alikuwa ameitengeneza.

Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na ligi nyingine mbalimbali hapa nchini na duniani, zimesimama ili kupambana na maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19), ambavyo vinaisumbua dunia kwa sasa.

Akizungumza na gazeti hili juzi, Mingange alisema uamuzi wa kusimamishwa ligi ulichukuliwa kwa misingi ya kina, lakini ana mashaka na vijana wake kurejea kwenye kasi ambayo walikuwa nayo kabla ya uamuzi huo kutolewa.

Mingange alisema licha ya kuwapa wachezaji wake maagizo ya kufanya katika muda huo wa mapumziko, hana imani watakaporejea kama watakuwa kwenye ubora wa kuhimili ushindani wa ligi hiyo iliyoko katika hatua ya lala salama.

"Licha ya kuwapa mikakati ya kufanya wanapokuwa nyumbani, lakini bado nitahitajika kufanya kazi kubwa ya ziada ili kuhakikisha wanarejea katika kasi yao ya awali ili kupambana kupata matokeo katika michezo yetu yote," alisema Mingange.

Alisema anahitaji kutoka katika nafasi walipo katika msimamo wa ligi ili kujinasua kwenye janga la kushuka daraja.
Ndanda ipo nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 31 zilizotokana na mechi 29.

Habari Kubwa