Kodi nyasi bandia yafutwa, kubeti...

11Jun 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kodi nyasi bandia yafutwa, kubeti...

SERIKALI imependekeza kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye nyasi bandia kwa viwanja vya mpira wa miguu katika majiji kwa ajili ya kuendeleza michezo na kukuza vipaji nchini.

Akiwasilisha Mapendekezo ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22 Bungeni jijini Dodoma jana, kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema kwa mwaka huu wa fedha, anapendekeza kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye nyasi bandia kwa ajili ya viwanja vya mpira wa miguu vya majiji, huku kukiwa na lengo la kufanya hivyo kwenye manispaa hadi kwenye timu wakati wa bajeti zijazo.

"Mheshimiwa Spika, viwanja vyetu vingi ni vibovu sana, labda ukiacha kile cha Majaliwa Lindi. Vingi ni vibovu. Na ubovu wa viwanja hivyo unasababisha timu bora kama Yanga inashindwa kupata matokeo mazuri inapokwenda mikoani," alisema waziri huyo na kusababisha vicheko na makofi kutoka kwa baadhi ya wabunge.

"Napendekeza kusamehe ongezeko la thamani kwenye nyasi bandia zinazotambulika kwa HS Code 5703.30.00 na 5703.20.00 kwa ajili ya viwanja vya mpira vilivyoko kwa kuanzia kwenye majiji.

Msamaha huo utahusisha ridhaa kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Ni jambo ambalo Waziri wa Sekta hiyo amelipigania sana. Lengo la hatua hii ni kuendeleza michezo na kukuza vipaji hapa nchini. Tukifanikiwa kwenye majiji, bajeti zinazofuata tutakwenda manispaa, kwenye viwanja hadi kwenye timu," alisema Dk. Nchemba.

Waziri huyo amependekeza pia kufanya mabadiliko ya Sheria ya Michezo ya Kubahatisha kupunguza kiwango cha kodi kwenye zawadi ya ushindi kutoka asilimia 20 hadi 15 na kuongeza kodi katika michezo ya Kubahatisha ya ubashiri wa matokeo ya michezo kwa mapato ghafi kutoka asilimia 25 ya mauzo ghafi hadi asilimia 30. Ongezeko tano litapelekwa kwenye mfuko wa Maendeleo ya Michezo kwa ajili ya kuendeleza michezo nchini.

Habari Kubwa