Kongamano la Soka lamrejesha Sven Dar

23Feb 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kongamano la Soka lamrejesha Sven Dar

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, Sven Vandenbroeck, anatarajiwa kurejea nchini kwa ajili ya kushiriki kongamano la soka linalotarajiwa kufanyika Machi 18 na 19, mwaka huu kwenye Ukimbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Sven, raia wa Ubelgiji alitangaza kuachana na Simba hivi karibuni na sasa amejiunga na klabu ya FAR Rabat ya Morocco.

Akizungumza na jijini jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Afrisoccer, Peter Simon, alisema maandalizi ya kongamano hilo yamekamilika na linatarajiwa kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa soka kutoka nchi mbalimbali akiwamo kocha huyo wa zamani wa Simba.

Simon aliwataja baadhi ya wageni wengine waliothibitisha kuhudhuria kongamano hilo ni pamoja na mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Senegal, Khalilou Fadida ambaye aliwahi kuichezea klabu ya Bolton Wanderers na Inter Milan, Marcos Pelegrín kutoka Afrika Kusini ambaye ni Mwakilishi wa Laliga na Mshauri wa Yanga, Senzo Mbatha.

Wengine watakaoshiriki ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, Mulamu Nghambi ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Simba, Abdulkarim Amin 'Popat' kutoka Azam FC na Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Wanawake Tanzania (TWFA), Amina Karuma.

"Mkutano huo utakuwa na wadau mbalimbali wa soka kutoka ndani na nje ya nchi, na lengo la kongamano hilo ni kutengeneza jukwaa la kuwawezesha wadau kujifunza na kubadilishana ujuzi na uzoefu."

"Pia kuainisha fursa mbalimbali za kibiashara na kujadili mambo muhimu yanayohusu maendeleo ya mpira wa miguu na kutengeneza uhusiano na ushirikiano," alisema Simon.

Alisema kongamano hilo litasaidia wadau wa hapa nchini kujifunza mbinu mpya za uendeshaji wa soka kupitia kwa wageni ambao nchi zao zimepiga hatua katika mchezo huo.

Aliongeza walengwa wa kongamano hilo la kwanza la kimataifa ni wadau wote wa soka hapa nchini wakiongozwa na Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kamati za Michezo za Mikoa na Wilaya, TFF, Bodi ya Ligi, klabu zote za soka, makocha na wachezaji wa zamani.

"Pia ni jukwaa muhimu kwa 'maskauti', waandishi wa habari za michezo na vituo vya soka," Simon aliongeza.

Alimtaja mgeni rasmi katika kongamano hilo atakuwa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa huku Katibu wake, Hassan Abbas atafunga kongamano hilo.

Habari Kubwa