Kuogelea ya taifa kuanza leo

10Apr 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Kuogelea ya taifa kuanza leo

MASHINDANO ya Taifa ya kuogelea yanatarajiwa kufanyika kuanzia leo kwenye bwawa la kuogelea la klabu ya Gymkhana Dar es Salaam na yatashirikisha wachezaji kutoka katika klabu sita za Tanzania Bara.

Mashindano hayo yanatarajia kushirikisha zaidi ya waogeleaji 90 wa Tanzania Bara na yamepangwa kufanyika kuanzia saa 2.00 asubuhi.

Waogeleaji hao watashindana  katika matukio 60 kwa katika staili za Freestyle, Butterfly, Backstroke, Breaststroke na Individual Medley. Pia watashindana katika relays.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Hadija Shebe alisema siku ya kwanza ya mashindano hayo waogeleaji watashindana katika matukio 60 na siku ya pili washiriki watashindana katika matukio 43.

Shebe alizitaja klabu ambazo zitashiriki katika mashindano hayo kuwa ni Dar es Salaam (DSC), Taliss, Bluefins, Mwanza, FK Blue Marlins na Mis Piranhas ya Morogoro.

Alisema wanatarajia kuwa na mashindano yenye upinzani na msisimko mkubwa kutokana na waogeleaji wanaoshiriki kufanya maandalizi vizuri.

“Klabu nyingi zimeleta waogeleaji wakali ambao mbali ya kuwania ushindi, pia wanapigania nafasi ya kuchaguliwa kwenye timu mbalimbali za Taifa ambazo zitashiriki mashindano ya kimataifa,” alisema kiongozi huyo.

Habari Kubwa