Kwasi afunguka  makohozi Yondani

01May 2018
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kwasi afunguka  makohozi Yondani
  • ***Jela, faini zinamhusu beki huyo wa kati wa Yanga baada ya TFF...

WAKATI ikielezwa beki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani, huenda akakumbana na adhabu ya kufungiwa mechi mbili na faini juu ama zaidi kutokana na kitendo chake cha kumtemea mate ('makohozi') beki wa Simba, Asante Kwasi,...

....timu hizo mbili zilipokutana juzi katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Mghana huyo amesema "yaliyotokea namwachia Mungu".

Katika mechi hiyo ya watani wa jadi ambao wanadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, Simba waliibuka na ushindi wa bao 1-0 Uwanja wa Taifa juzi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Saloum Chama, alisema kwamba alishuhudia kitendo hicho, lakini kamati yake itatoa uamuzi kwa kuzingatia ripoti ya mwamuzi, kamisaa au ushahidi wa picha za video ambazo zitawasilishwa.

Chama alisema, pia kwa kuzingatia uzito wa tukio lililojitokeza, kamati yake inaweza kumsimamisha kwa muda na kulipeleka katika Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili wachukue hatua ambayo wanaamini itakuwa ni fundisho kwa wachezaji wengine wasirudie.

"Kanuni zinasema kosa kama lile ni kufungiwa kati ya mechi moja au mbili au kupigwa faini, au kupata adhabu zote kwa pamoja, na kwa kuangalia uzito wa jambo husika, tunaweza kumsimamisha na kumpeleka katika Kamati ya Nidhamu," alisema Chama ambaye pia ni mwamuzi mstaafu.

KWASI AFUNGUKABeki huyo raia wa Ghana alisema anashukuru timu yake imepata ushindi katika mechi hiyo, lakini anamwachia Mungu kitendo alichofanyiwa na Yondani.

"Habari za asubuhi kila mmoja wenu, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa ushindi ambao ametupa jana (juzi), jina lake litukuzwe,... kilichonitokea jana (juzi) hakikuwa kitendo kizuri, lakini napenda kusema ninamwachia Mungu, " alisema Kwasi.

Hata hivyo, Yondani jana hakuweza kupatikana katika simu yake ya mkononi ili kuelezea kama alifanya kwa makosa au alidhamiria.

LENCHATRE HAKURIDHIKAWakati timu yake ikiwa inatembea na harufu ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu wa 2017/18, Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre, amesema kikosi chake kilistahili kupata ushindi mnono katika mechi hiyo dhidi ya watani zao.

"Kama wachezaji wangu wasingekuwa na papara, wangefunga mabao matatu au manne, lakini huo ndio mpira ulivyo, tunashukuru tumepata pointi tatu na kimahesabu tunahitaji pointi nne tu ili tutangazwe kuwa mabingwa," alisema Mfaransa huyo.

 

Habari Kubwa