Lete Raha Miss Tanzania yatoa msaada Hospitali Dodoma

08Oct 2016
Faustine Feliciane
Dodoma
Nipashe
Lete Raha Miss Tanzania yatoa msaada Hospitali Dodoma

WASHIRIKI wa shindano la kumsaka mrembo wa Tanzania 'Lete Raha Miss Tanzania 2016' jana walitoa msaada kwa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa Dodoma.

Washiriki wa shindano la Lete Raha Miss Tanzania 2016, wakifanya usafi katika Hospitali ya Rufaa Dodoma jana. PICHA: HALIMA KAMBI

Warembo hao walitoa msaada wa vifaa mbalimbali kwenye wodi ya kina mama waliojifungua ambapo pia walifanya usafi hospitalini hapo.

Akizungumza wakati akiwapokea warembo hao hospitalini hapo, Kaimu Mganga Mkuu, Caroline Damian, aliwata warembo hao kujitambua kuwa ni kioo cha jamii katika ngazi mbalimbali na kujitolea kwa ajili ya watu wenye mahitaji muhimu.

"Nawakaribisha sana Dodoma, ninyi nyote ni washindi hata kama atahitajika kupatikana mmoja kwenye fainali..., mnatakiwa kujitambua kuanzia sasa na mfanye mambo yatakayoonyesha thamani na umuhimu wa shindano hili," alisema Caroline.

Alisema hata msaada walioutoa kwa kina mama waliojifungua hospitalini hapo umeonyesha uthamani mkubwa kutoka kwa warembo hao.

"Kwa kweli sisi kama wafanyakazi wa hospitali, tumefurahishwa sana na hatua ya kuja hapa na kutoa msaada kwa akina mama hospitalini hapa, naamini hata wao wenyewe wamefurahi sana," aliongezea kusema Caroline.

Warembo hao walikabidhi vitaulo vya kike (Pad) maalum kwa kina mama waliojifungua vilivyotolewa na Kampuni ya NN General Supplies Co, Ltd.

Shindano la mwaka huu limedhaminiwa na Kampuni ya The Guardian Ltd kupitia gazeti lake la Michezo na Burudani la Lete Raha, wadhamini wengine ni pamoja na PII, Morena Hotel Dodoma, Regency Park, Dodoma Carnival, HC, pamoja na Jizi Lounge Msasani.

Fainali za shindano hilo imepangwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu jijini Mwanza.

Habari Kubwa