Ligi Kuu Bara bila mashabiki

23May 2020
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
Ligi Kuu Bara bila mashabiki
  • Yapangwa kuchezwa katika vituo, Sh. milioni 417 zatengwa kwa ajili ya posho na malazi...

SERIKALI imetangaza kutenga kiasi cha Sh. milioni 417 kwa ajili ya kuziwezesha timu zinazoshiriki ligi mbalimbali nchini kumalizia msimu wa 2019/20 ambao ulisimama ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona (COVID 19), imefahamika.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye jana jijini Dodoma alitoa ufafanuzi kuhusiana na kurejea kwa Ligi Kuu Bara. PICHA: MAKTABA

Akizungumza jijini hapa jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alisema wameamua kutoa fedha hizo ili kuzisaidia timu gharama za uendeshaji baada ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kutangaza kufungua michezo hapa nchini.

Mwakyembe alisema serikali kwa kushirikisha na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Nchini (TPLB), ziliona haitakuwa na tija kama wataziacha timu bila ya kuwasaidia katika kipindi hiki chenye changamoto.

“Kwa maana hii sasa, serikali kwa kushirikina na Tff, Bodi ya Ligi pamoaja na wadhamini, wameamua kutoa kiasi hichi cha fedha ili kuziwezesha timu hizi kumaliza mashindano na msimu wa mwaka 2019/20,” alisema Mwakyembe.

Alisema wataanza na michezo ya Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili na mashindano ya Kombe la FA na ligi hizo zitachezwa katika vituo viwili vya Dar es Saalam na Mwanza ili kupunguza gharama za uendeshaji.

“Kiasi hichi cha fedha kitatumika katika kuziondolea gharama timu kama vile posho za wachezaji, malazi pamoja na chakula, hatutaki kusikia kuna timu imekosa chakula wakati ligi imeanza, ndio maana tumeondoa ule mfumo wa nyumbani na ugenini ili kupunguza gharama katika kipindi hicho cha corona,” Mwakyembe alisema.

Alisema kituo cha Dar es Saalam kitahusisha mechi za Ligi Kuu na michuano ya Kombe la FA kwenye Uwanja wa Taifa, Azam Complex na Uhuru wakati Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili zitachezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba na Nyamagana jijini Mwanza.

Aliongeza pamoja na serikali kuruhusu michezo irejee, lakini itaendelea kuchukua tahadhari katika maeneo yatakayohusisha michezo hiyo ili kujikinga na corona.

“Wachezaji wote watakaoshiriki michezo watapimwa joto kabla ya mechi kuanza, lakini pia mashabiki kwa kipindi hiki hawataingia uwanjani, tunaangalia uwezekano wa kuruhusu idadi fulani ya mashabiki kama vile vikundi vya ngoma ili uwanja usiwe kimya kabisa,” aliongeza Mwakyembe.

Aliliagiza Baraza la Michezo Tanzania (BMT), kuanza kuweka taratibu mbalimbali kuhusiana na usimamizi wa michezo mingine ambayo itafanyika hapa nchini.

Alisema pia Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC), huenda kikaonyesha mechi za Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili katika kipindi hiki ambacho mashabiki hawaruhusiwi kuingia viwanjani.

Habari Kubwa