Ligi Kuu Bara Sept. 29

05Aug 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ligi Kuu Bara Sept. 29
  • ***Bodi ya Ligi yafunguka viporo sasa itakuwa historia katika msimu ujao...

MSIMU mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara wa mwaka 2021/22 ambao utashirikisha timu 16 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini umepangwa kufanyika kuanzia Septemba 29, mwaka huu imefahamika.

Simba ya jijini Dar es Salaam ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo, ikishinda taji hilo kwa misimu minne mfululizo.

Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania, Almasi Kasongo, alisema Ligi Kuu itaanza rasmi baada ya mchezo wa Ngao ya Hisani utakaochezwa ifikapo Septemba 25, mwaka huu kwa kuwakutanisha watani wa jadi, Simba na Yanga.

Kasongo alisema mechi hiyo ya Ngao ya Hisani itachezwa kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na wanazitaka timu husika kujiandaa vyema kwa sababu wanafahamu mchezo huo unavuta hisia za wadau mbalimbali wa soka kutoka ndani na nchi jirani ya Tanzania.

Alisema ratiba kamili ya msimu mpya itatolewa hivi karibuni na itakuwa iliyokamilika ili timu ziweze kufanya maandalizi na kujiweka tayari na msimu huo mpya.

Kiongozi huyo alisema wanatarajia msimu mpya hautakuwa na mechi za viporo kwa sababu timu zote zitakuwa zinacheza kila raundi kwa wakati mmoja na kwa kufanya hivyo, ushindani uliokusudiwa kwenye ligi hiyo ya juu nchini utaonekana.

"Ligi yetu rasmi tutaifungua rasmi Septemba 25, ni mazingatio yetu na mwelekeo wetu kuwa na viporo sifuri, tusiwe na viporo kabisa, baada ya majadiliano marefu, mazungumzo sahihi, kwa kauli moja tumekubaliana na vilabu, ligi itakuwa inasisimama pale klabu nyingine zitakazokuwa na mechi za kimataifa," alisema Kasongo.

Aliongeza uamuzi huo umepata baraka kutoka kwa klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu na msingi huu umefikiwa baada ya kufahamu msimu ujao Tanzania itawakilishwa na timu nne katika mashindano ya kimataifa yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Alisema pia katika kikao cha pamoja na vilabu, wamefanyia maboresho kanuni ikiwamo kupata uwakilishi wa timu pale nchi inapopata nafasi nyingi kwenye michuano ya kimataifa na maboresho ya viwanja vitakavyotumika.

"Pia tumeziangalia kanuni ambazo zitasimamia yale yasiyopendeza, tuwe na ligi yenye weledi na adhabu kulingana na makosa yanayojirudia," Kasongo alisema.

Alieleza pia msimu ujao, timu zitakuwa zinapumzika siku tatu baada ya kutoka kwenye michezo ya kimataifa badala ya sita kama ilivyokuwa katika msimu uliopita na kwa kuzingatia hivyo, kalenda yetu itakwenda vizuri.

Timu zitakazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao ni pamoja na mabingwa Simba, Yanga, Azam FC, Biashara United, KMC FC, Tanzania Prisons, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Ruvu Shooting, Polisi Tanzania, Dodoma Jiji, Namungo FC, Mbeya City, Coastal Union, Geita Gold FC na Mbeya Kwanza.