Ligi Kuu Bara vumbi viwanja vitatu

07May 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Ligi Kuu Bara vumbi viwanja vitatu

LIGI Kuu ya Soka Tanzania Bara inatarajia kuendelea leo katika viwanja vitatu tofauti, huku mbio za kujiepusha na janga la kushuka daraja zikionekana kuwa na kasi kwa JKT Ruvu, Mgambo Shooting na Coastal Union.

Coastal Union

JKT Ruvu, ambayo Jumatano iliibana Azam FC ikitoka nyuma na kumaliza na sare ya mabao 2-2, leo itaikaribisha Ndanda FC kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi, mkoani Pwani na endapo itashinda itafikisha pointi 29 na kujiweka katika 'ahueni' ya kutoshuka daraja msimu ujao.

Kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga Stand United itacheza na mabingwa wa mwaka 1988 Coastal Union kutoka jijini Tanga ambayo inaburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kujikusanyia pointi 22 kati ya mechi 28 ilizocheza.

Ili ibaki kwenye ligi hiyo, Coasta Union inahitaji kushinda mechi zake mbili zilizobaki na pia kuziombea dua mbaya Mgambo Shooting yenye pointi 23, Kagera Sugar (25), Kagera Sugar na JKT Ruvu zenye pointi 26 zifungwe mechi zake zote zilizobakia.

Mechi nyingine ya ligi itakayochezwa leo ni kati ya Mgambo dhidi ya Mtibwa Sugar itakayofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa Simba kuikaribisha Mwadui FC kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, wakati Prisons itaivaa Majimaji mkoani Mbeya, huku Kagera Sugar wakicheza na Azam FC kwenye Uwanja wa CCM Kambarage.

Habari Kubwa